Tuesday 9 December 2014

WENYE ULEMAVU WASHIRIKISHWE KATIKA NIPANGO YA MAENDELEO

Watafiti wameeleza njia za kujenga uchumi jumuishi kwa wananchi wengi wakiwamo watu wenye ulemavu wakipendekeza kuwa mipango ya maendeleo iwashirikishe watu hao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Prof. Samuel Wangwe (pichani), aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uwasilishwaji wa ripoti ya matokeo ya utafiti kuhusu ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika mifumo ya Hifadhi ya Jamii.

Alisema utafiti umebaini kwamba sera na sheria za nchi zinawatambua watu wenye ulemavu, lakini ushirikishwaji kwenye mipango ya maendeleo bado ni mdogo.

“Utafiti huu unatoa ushauri kwamba watu wenye ulemavu washirikishwe kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo,” alisema.

Naye Dk. Flora Myamba, aliyefanya utafiti huo, alisema wamebaini kuwa ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye mipango mbalimbali ni mdogo akitolea mfano Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), unalenga kuwakomboa wananchi masikini, lakini haujataja kundi hilo kama watu masikini wenye mahitaji maalum, jambo linalowafanya wasifikiwe kikamilifu na mpango huo.

Alisema watu wenye ulemavu wana mahitaji maalum kwenye huduma mbalimbali kama afya akisema wanalipa ghali zaidi kuliko wasio walemavu.

“Imebainika kuwa watu wenye ulemavu wanalipa mara mbili ya gharama za matibabu yaani wanalipa Sh.  26,093 ikilinganishwa na Sh. 13,267 zinazolipwa na watu wengine kwa ugonjwa unaofanana,” alisema.

Alisema takwimu za watu wanaotumia mfumo wa bima ya matibabu kwenye Halmashauri (CHC), zinaonyesha kuwa watu wenye ulemavu ni wachache na kwamba hata huduma wanazopewa ni ndogo ambazo hazizingatii hali yao ya ulemavu.

Kwa upande wake, Meneja Utetezi kutoka Hospitali ya CCBRT, Frederick Mvigala, ambaye ana ulemavu wa viungo, alisema pamoja na kwamba Tanzania imeridhia mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, kundi hilo bado halijashirikishwa kikamilifu kwenye kuandaa sera na mipango mbalimbali ya maendeleo.

Alisema ni wakati sahihi sasa kwa serikali kulishirikisha kundi hilo kabla ya kuandaa mpango wowote ili kutambua mahitaji yao na kuyaweka kwenye utekelezaji.

Utafiti huo uliendeshwa katika Wilaya tatu za Nachingwea, Mbeya na Muheza.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!