Thursday 4 December 2014

WENYE ULEMAVU WAHAKIKISHIWA HUDUMA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge,  William Lukuvi, (pichani) amesema serikali itajitahidi kuhakikisha walemavu wanapata huduma muhimu kama watu wengine ili waweze kujiinua kichumi.



Akihutubia kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani ambayo kitaifa yalifanyika uwanja wa Kichangani mkoani hapa kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi alisema kuwa    ili kuinua uchumi wa taifa, lazima serikali iwaunge mkono walemavu kwa kuwapatia haki zao za msingi kwa kuwaboreshea miundombinu.

  Alisema kwa kupitia sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010,  serikali imeweka miongozo na namna ya kutekeleza na kutoa huduma kwao..

“Yapo mambo mengi ambayo serikali imefanya kwa kundi hili la walemavu, pia  mengine tunaendelea kuyafanya kwa ajili ya ustawi wao wa watu kama hawa,” alisema lukuvi Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Walemavu Tanzania    (Shivyawata), Amina Molel  aliiomba serikali kuifanyia mabadiliko sheria ya haki za watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 ili kulipa baraza lao la taifahaki zao stahiki.

“Baraza linatakiwa kuratibu, kusimamia na kutekeleza masuala yetu likiwa chombo huru badala ya kuwa chombo cha ushauri tu chini ya utendaji wa kamishna wa idara ya ustawi wa jamii ambaye kwa nafasi yake ana majukumu mengi, ” alisema Molel.

Alisema walemavu bado wanakabiliwa na changamoto nyingi  ambazo  ni  kutopatikana kwa taarifa muhimu katika mifumo iliyo rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Alizitaja changamoto zinazowakabili walemavu kuwa ni kukosekana kwa wakalima wa lugha ya alama kwenye vipindi vya televisheni, mijadala ya vikao vya bunge na hotuba za viongozi.

Nyingine ni  vyombo vya usafiri vya umma na majengo yanayotoa huduma kwa umma kutozingatia mahitaji ya walemavu, ruzuku ndogo kwa vyama vya walemavu ambayo hata hivyo kwa miaka mingi haijatolewa na kukosekana kwa uwakilishi katika vyombo vya maamuzi na kisera.

Kukosekana kwa ofisi ya kudumu ya shirikisho hilo na kucheleweshwa utoaji ardhi wilayani  Kibaha mkoa wa Pwani kwa lengo la kujenga chuo cha madereva na ufundi kwa walemavu.

Aliiomba serikali ilipatie shirikisho hilo  ofisi ya kudumu ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea pindi wafadhili wa nje watakapositisha kuwapatia kodi ya pango la ofisi.

Vilevile aliiomba  kuwaondolea kodi kwenye vifaa vya walemavu vinavyoingizwa nchini kama msaada. Mollel alisema kuondelewa kwa msamaha huo wa kodi, kutawawezesha walemavu wengi kupata vifaa vya kufanyia kazi kama kompyuta na  kurahisisha utendaji kazi wao.

Alisema kulingana na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo”Maendeleo Endelevu ahadi ya Teknolojia” inabidi walemavu wapate huduma za mtandao na  kuendana na wakati huu.

Hata hivyo, alisema wanaishukuru kwa kuthamini, kutambua na kuwaheshimu walemavu kwa kutekeleza madai wanayoiomba.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!