Friday 12 December 2014

WATOTO 47 000 HUFARIKI KILA MWAKA WAKATI WA KUZALIWA

Wakati serikali ikieleza kuwa  imefanikiwa kufikia  malengo ya Milenia namba nne mwaka 2015 kuhusu masuala ya afya, bado idadi ya vifo kwa watoto wachanga iko juu kwani kila mwaka Tanzania hupoteza takribani watoto 47, 000 ambao huzaliwa wakiwa wamekufa.

Pia wastani wa watoto wachanga  39, 000 huishi kwa mwezi mmoja tu baada ya kuzaliwa na hivyo kuifanya Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi  11 zenye idadi kubwa ya vifo vya watoto duniani.

Pia Tanzania imeendelea kupokea watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti) takribani 213, 500  kila mwaka na hivyo kuifanya kuwa ya 12 kwa kuwa  na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa wakiwa njiti.

Aidha, vifo vya watoto wachanga vinachangia asilimia 40 ya vifo vyote vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano nchini huku sababu zinazochangia vifo hivyo zinaweza kuzuilika.

Hayo yalibainishwa jana katika mkutano wa wadau wa afya  kutoka ndani na nje ya nchi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam ili kujadili mikakati mbalimbali ya namna ya  kudhibiti vifo kwa watoto wachanga nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma  za Kinga kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Neema Rusibamayila,  alisema, Tanzania imefanikiwa kufikia malengo ya milenia namba nne ya mwaka 2015 katika kupunguza ongezeko la vifo kwa watoto wachanga, lakini kasi yake ni ndogo kwani takwimu za sasa zinaonyesha kuwa takribani watoto 47, 000 huzaliwa wakiwa wameshakufa nchini.

Alisema, vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa kiwango kikubwa, lakini maendeleo yamekuwa ya kasi ndogo kwenye uhai wa watoto wachanga.

Dk. Rusibamayila alitaja baadhi ya sababu zinazochangia vifo hivyo kuwa ni pamoja na watoto kuzaliwa wakiwa njiti, kukosa pumzi na kuwa na maambukizi mbalimbali ya magonjwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!