Sunday, 28 December 2014

WALIMA MAPARACHICHI KUPATIWA SOKO UARABUNI

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amesema anaendelea na jitihada za kutafuta soko kwa matunda aina ya parachichi katika nchi za Mashariki ya Kati ambako mahitaji yake ni makubwa.

Hata hivyo, alisema ili kupata soko la uhakika na la kudumu, wakulima hao wanapaswa kubadili kilimo ili kiwe cha kisasa kitakachotoa mazao kwa wingi.
Akizungumza alichojifunza katika ziara ya siku 10 katika nchi za Qatar, Dubai na Falme za Kiarabu ambako alikuwa kwenye msafara wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mkuu huyo wa mkoa alisema umefika wakati sasa kwa wakulima kuwaza masoko ya nje ya nchi badala ya yale yaliyoko jijini Dar es Salaam tu.
“Ziara hii imenifungua, nikirudi nitatumia nafasi hii kuwasaidia wakulima kulima mazao bora na nitasimamia kuhakikisha wanapata masoko ya nje, hasa Falme za Kiarabu ambako kuna mahitaji makubwa ya mazao mbalimbali ambayo tunayazalisha.
“Mbeya tunalima sana maparachichi na pia tuna machimbo ya mawe ya malumalu (mables) kwa wingi, kwa Falme za Kiarabu, parachichi na hizi malumalu zinahitajika sana, ni kiasi cha kuwaambia wakulima wayalime kwa wingi na wengine wachimbe malumalu kwa ubora watapata soko tu na itawasaidia sana,” alisema.
Hata hivyo, alionyesha wasiwasi wa namna ya usafirishaji. “Hii ni ajenda muhimu inapaswa tuifanyie kazi mapema kabla ya kuanza kuwahimiza,” alisema Kandoro.
“Tutashirikiana, tutasaidiana katika kupakia kisasa zaidi ili kulifikia soko la kimataifa kwa ubora unaostahili. Bahati nzuri tuna Uwanja wa Ndege wa Songwe na vinginevyo tutasafirisha kwa barabara hadi Dar es Salaam na kupelekwa Arabuni,” alisema mkuu huyo wa mkoa

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!