Sunday 7 December 2014
VIONGOZI WA DINI TOENI MATAMKO YENYE TIJA"
KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa nchini ambayo kwa namna moja ama nyingine yamehusisha mamlaka za kiserikali, kisiasa na kijamii.
Katika matukio hayo tumeshuhudia watu kadhaa wakitoa matamko yao kama njia ya kuwasihi wananchi na kuwataka kuwa watulivu wakati masuala mbalimbali yakichukuliwa hatua.
Kati ya viongozi ambao kwa nafasi yao katika jamii na kuaminika kwa wananchi wamekuwa wakitoa matamko ni viongozi wa taasisi mbalimbali za dini ambao wamekuwa wakitoa matamko kwa lengo la kuwataka wananchi kutulia na kutafakari kwa umakini kuhusu jambo fulani.
Hata hivyo, wakati fulani taasisi hizo za dini zimekuwa zikionekana kuegemea upande mmoja huku baadhi ya waumini wakiwatafsiri vibaya na kuonekana kama wanatumika na upande wanaoutetea.
Mimi naona kwa nafasi ya viongozi wa dini na taasisi zao kutoa matamko ya namna yoyote kwa jamii si jambo baya na muhimu sana kwani wakati fulani inasaidia kupunguza hasira au sintofahamu kwa baadhi ya wananchi.
Lakini kwa upande mwingine ni vyema viongozi au taasisi za dini kuwa makini pale wanapotoa matamko na kama ikionekana kunaweza kusababisha vurugu ni vema kukaa kimya kwani viongozi wa dini ni watu wanaoheshimika katika jamii.
Iwapo kutatokea tamko ambalo linaweza kuleta utata kwa jamii badala ya kuwatuliza wananchi linaweza likachochea na kuwa chanzo cha kukosekana kwa amani miongoni mwa jamii husika.
Nasema hivyo kutokana na matamko kadhaa yaliyowahi kutolewa na baadhi ya taasisi za dini na kusababisha vurugu hususani kwa masuala ya kisiasa, kwani iwapo kiongozi wa taasisi husika anataka kutoa tamko kuhusu suala husika ni vema kulielewa na kuwa na uhakika na anachokisema ili kutoruhusu mkanganyiko kwa wahusika.
Si kwamba wote wanaotoa matamko wanakuwa wameegemea upande fulani na kusababisha sintofahamu bali ni ukweli pasipo shaka kwamba wapo ambao kwa kiasi fulani bila kufanya utafiti wa kina wa nini kinahitajika kuzungumzwa na matokeo yake yatakuwaje, wamekuwa wanachochea migogoro badala ya kuitafutia ufumbuzi.
Napenda pia kuviasa vyombo vya habari kuwa makini na matamko hayo kama wanaona hayana tija kwa jamii ni vema kuacha kabisa ili kuhakikisha amani na imani kwa kiongozi au taasisi husika inabakia kulinda maslahi ya nchi.
Hivyo ninawasihi viongozi wa dini na taasisi zake kuwa makini na matamko yao kwa kujipima mara mbili kwani ukitoa tamko ambalo waumini wako hawataelewa utakuwa umepunguza heshima yako kwa jamii na kuonekana kama umetumika.
Hata siku nyingine ukiwa na tamko zuri la kujenga, ni dhahiri wataona kama hauko makini na jambo unalojadili na kamwe si vema kukubali kutoa tamko hata kama ni kwa maslahi ya jamii ikiwa huna uhakika nalo.
Wananchi pia wanatakiwa kutafakari na kufanyia kazi matamko ya watu wa dini kwa lengo la kujenga na kulinda amani iliyodumu tangu uhuru badala ya kushabikia matamko yanayoweza kusababisha vurugu kwa jamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment