Akikumbuka madhila anayokumbana nayo, anasema hana hamu na wanaume kutokana na kile alichofanyiwa na mwanaume aliyewahi kuishi naye miaka.
Stella, anayeishi eneo la Msimba wilayani Kilosa, anasema mikasa ya maisha magumu anayopata sasa ilianza baada ya kukimbiwa na mwanaume baada ya kujifungua mtoto mlemavu wa viungo. Ifuatayo ni simulizi yake:
“Mtoto wangu anaitwa Meshack, baba yake alimkimbia baada ya kugundua ni mlemavu, amepooza mguu na mkono na niligundua kuwa ni mlemavu wa viungo baada ya mwaka mmoja. Pia hawezi kuongea mpaka sasa unavyomuona ana umri wa miaka nane hawezi kuita hata mama.
“Baada ya kugundua mtoto ni mlemavu mume wangu akaanza kunichukia na ndipo akakosa mapenzi ya mtoto na kukimbia. Ameondoka kijijini ameenda kuishi Morogoro mjini, na hatuna mawasiliano yoyote.
“Siku za nyuma mtoto alipozaliwa alikuwa anatoa huduma za mtoto, lakini tangu mtoto alivyogundulika ni mlemavu, sijaona msaada wake mpaka leo. Ninamtunza mtoto wangu mwenyewe, sijui wazazi wake wala ndugu zake.
“Tulikutana huku Msimba, na hakuwahi kunionyesha ndugu zake zaidi ni kaka yake mmoja ambaye siku za mwanzo nilimfuata na kumueleza, lakini alipuuzia na hakunipa msaada wowote. Sina msaada wowote zaidi ni mimi nahangaika na biashara yangu ya mkaa ndio inayonisaidia kumtunza mtoto wangu.”
Changamoto za malezi
Kwa kuwa ulemavu wa Meshack ni mkubwa, anahitaji uangalizi wa ziada na wa karibu. Anasema mara kwa mara anaumwa, hata shule ameshindwa kumpeleka kwa sababu hajimudu, wakati yeye analazimika kufanya kazi zaidi ili kumtimizia mahitaji muhimu.
Anachoshukuru Stella ni kuwa katika jamii anayoishi licha ya kukosa msaada wa kumwezesha kuishi na mtoto wake, majirani na ndugu katika hawamnyanyapai mwanawe, jambo linalompa faraja.
“Watoto wenzake wanacheza nae na wanajua kuwa mwenzao ni mlemavu, na kuna wakati wanamsaidia. Wameshamzoea kwa kuwa wameishi nae mwaka wa nane huu,’’ anaeleza.
Swali: Kilichomsimbu mwanao, labda uliwahi kukigundua ulipokuwa mjamzito?
Jibu: Ndio kipindi nina mimba nilikuwa naumwa malaria mara kwa mara, simalizi mwezi lazima niumwe. Hali ile ilinifanya nidhoofike sana hadi wakati najifungua Meshack.
Swali: Ulishawahi kumpeleka hospitali kwa matibabu?
Jibu: Nilimpeleka Hospitali ya Ifakara, wakanielekeza niende Morogoro kwenye kituo cha walemavu. Nilikaa pale kwa miezi mitatu, alikuwa akifanyiwa mazoezi ya viungo ambayo yalimsaidia kuanza kutembea kidogo kidogo alivyofikisha miaka mitano. Hata hivyo hajaweza kukaza kutembea kama walivyo watoto wengine.
Swali: Baada ya kukimbiwa na mume wako, uliwahi kuripoti sehemu yoyote kwa ajili ya msaada wa kisheria?
Jibu: Hapana, nimepuuzia. Niliamua mwenyewe kupambana na mtoto wangu hadi dakika za mwisho. Nikiwa kama mwanamke nafanya kazi kwa bidii, kuhakikisha mwanangu anakula, anavaa na anapata mahitaji yale muhimu. Mungu atanilipia, yeye kamkimbia mtoto lakini amesahau yote ni mipango ya Mungu na yeye siku moja anaweza kuwa mlemavu tena zaidi ya huyu Meshack.
Swali: Una mpango wowote wa kuolewa?
Jibu: Sina mpango wowote, nawachukia wanaume. Wote nawaona ni wale wale kama baba yake Meshack. Kwa kweli nawachukia kutoka moyoni, inasikitisha kumkimbia mchumba, mke wako kisa tu kazaa mlemavu. Huyu mtoto ni wetu sote, anahitaji mapenzi ya baba na mama. Kutokana na alichonifanyia baba yake Meshack, nimewachukia wanaume na kamwe sitotaka kuolewa.
Swali: Unawambiaje wanaume?
Jibu: Nawambia wanaume wote wamuogope Mungu.
, wanachofanya ni kinyume na mapenzi ya Mungu. Hakuna mwanamke ambaye anapenda kuzaa mtoto mlemavu kama Meshack, hali kama hii inaweza kumpata mtu yoyote bila ya kuzingatia umri au jinsia. Wanaume wanatakiwa kuwa na utu, wawaheshimu wake zao na kuwapenda watoto.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment