Tuesday 9 December 2014

NYERERE ALIVYOHAHA KUWAHI UWAZIRI MKUU-MZINDAKAYA


MWANASIASA mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya amesema njia ya pekee ya Watanzania kuenzi mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali tangu nchi ijipatie uhuru wake miaka 53 iliyopita, ni kuhakikisha amani, utulivu na mshikamano uliopo unalindwa na kudumishwa kwa gharama yoyote ile.


Dk Mzindakaya, mmoja wa viongozi wastaafu wanaoheshimika nchini, pia ameelezea jinsi nchi ilivyotoka mbali na hata kupata mafanikio baada ya Uhuru mwaka 1961.
Alisema hayo hivi karibuni katika mahojiano maalumu mjini Sumbawanga alipokuwa anazungumzia miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika inayoadhimishwa leo.
Alisema nchi ilikuwa taabani, ikikosa hata barabara za uhakika, hali iliyomlazimu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere licha ya kuwa nchini, alilazimika kupita nchini Zambia kwenda Dar es Salaam baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika.
Alisema anakumbuka mwaka 1959 wakati Mwalimu Nyerere akiwa mjini Sumbawanga, Gavana Edward Twinning alimteua kuwa Waziri Mkuu hivyo ilimlazimu kusafiri hadi Zambia ambako alipanda ndege kwenda Dar es Salaam.
“Ilitulazimu tumkimbize hadi nchini Zambia ili aweze kupanda ndege. Isitoshe kabla ya Uhuru ukitaka kusafiri kwenda Dar kwa ndege kutokea Mbeya ilitulazimu kupitia Mwanza kisha Dar.
Aliendelea kusimulia, “wakati huo, kulikuwa na ndege iliyojulikana kama Grasshopper, yaani Panzi ilikuwa na kasi ndogo sana safari ya Mbeya – Dar ilichukua saa sita na ile ya Mwanza hadi Dar saa tano.“
Mzindakaya ambaye pia ni maarufu kama `Kamusi’ ya Historia ya Mkoa wa Rukwa, alisema ni shuhuda wa mafanikio makubwa ambayo nchi imejipatia.
Alisema kwamba kabla ya Uhuru kulikuwa hakuna barabara iliyokuwa ikiunganisha Mji wa Sumbawanga na Mji Mdogo wa Tunduma.
“Wakati huo sisi tuliokuwa tukiishi Sumbawanga tulilazimika kupitia Mbala nchini Zambia ili tuweze kufika Tunduma wakati tukisafiri kwenda Dar… safari iliyochukua takribani wiki nzima kutokana na kutokuwepo kwa barabara kutoka Sumbawanga hadi Tunduma. “Barabara hii iliitwa barabara ya mzimu kutokana na ubovu wake,” alibainisha akisisitiza kuwa sasa ni tofauti nchi karibu yote imeunganishwa na mtandao wa barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
Kuhusu sekta ya elimu, alisema imepiga hatua kubwa hasa baada ya Azimio la Musoma, kwani kwa sasa karibu kila kijiji kina shule ya msingi na vingine vina zaidi ya shule moja na pia shule za sekondari zimeongezeka takribani kila kata. Hali kadhalika, vyuo vikuu vimeongezeka kutoka sifuri kabla ya Uhuru hadi kufikia 40 kwa sasa.
Alitaja Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kilichojengwa na Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kinatarajiwa kuwa cha kipekee kwa ukubwa katika nchi za Mashariki mwa bara la Afrika.
Kwa upande wa huduma za jamii alisema mafanikio yanaonekana yenyewe takribani kila kijiji nchini kina zahanati na vituo vya afya vimejengwa kila kata nchini.

CHANZO.HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!