Thursday 4 December 2014

NUSU YA WAKAZI WA DAR KUTOPIGA KURA DESEMBA 14



ASILIMIA 42 ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam ndiyo waliojitokeza kujiandikisha kwa ajili ya upigaji kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, utakaofanyika Desemba 14, mwaka huu.



Imeelezwa kuwa kati ya wapigakura 1,679,726 wenye sifa ya kujiandikisha, ni 704,002 tu ndiyo wamejiandikisha, sawa na asilima 42.

Sababu kubwa imetajwa ni pilika za maisha miongoni mwa wakazi wa jiji hilo, ambao mara nyingi hutoka alfajiri na kurejea nyumbani usiku, muda ambao vituo vya kuandikisha vinakuwa vimefungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari. Alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala lengo lilikuwa kuandikisha watu 329,726, lakini waliojiandikisha ni 184,850, sawa na asilimia 56.1.
Kinondoni walengwa walikuwa 850,000, lakini waliojiandikisha ni 272,869 sawa na asilimia 32, wakati kwa Temeke lengo lilikuwa kuandikisha watu 500,000, lakini walijitokeza ni 246,283 sawa na asilimia 49.2.
Uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulifanyika kwa wiki moja kuanzia Novemba 23 mwaka huu. Kwa mujibu wa ratiba ya mchakato wa uchaguzi, vyama na wagombea sasa wapo katika kipindi cha kampeni hadi Desemba 13, siku moja kabla ya uchaguzi.
Akizungumzia changamoto walizokumbana nazo katika uandikishaji, alisema mbali na watu wengi kutojitokeza, pia kulikuwa na migogoro ya mipaka katika baadhi ya mitaa mipya ya Turiani na Kigezi kata ya Buyuni na Kiboga na Kichangani Kata ya Kinyerezi kwa upande wa Ilala.
Alisema nafasi zinazowaniwa ni wenyeviti wa mitaa 559 na wajumbe wa kamati za mitaa 2,795, ambapo sasa uhakiki wa majina unaendelea katika ofisi husika.
Pia, alisema mawakala wa vyama vya siasa walikuwa chanzo cha vurugu katika kujiandikisha katika baadhi ya vituo vya kujiandikisha. Alitoa mwito kwa vyama kufanya kampeni za kistaarabu.
Aidha, alikumbusha kuwa siku ya uchaguzi, vyama vya siasa haviruhusiwi kufanya kampeni; na kwa siku za kampeni, muda unapaswa kwisha ifikapo saa 11 jioni, kinyume cha hapo wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Maabara za JK Akizungumza utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuhakikisha kila shule ya sekondari ya Kata, inakuwa na maabara tatu za masomo ya sayansi kabla ya mwishoni mwa mwezi uliopita, alisema Dar es Salaam imekamilisha ujenzi huo kwa asilimia 97.
Alisema maabara 274 kati ya 281 zimejengwa na kufikia hatua mbalimbali za ukamilishaji, zikiwemo uwekaji masinki, mifumo ya maji safi na majitaka, umeme, meza na vifaa vya maabara.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!