Thursday 4 December 2014

NAMNA YA KUFANYA BIASHARA KWA FAIDA

Tumekuwa tukisoma na hata kusikia mazungumzo ya kawaida na kwenye vyombo vya habari juu ya ndoto za wajasiriamali mbalimbali wakisema wanataka kuwa kama mfanyabiashara fulani maarufu kutokana na biashara wanazozifanya.

Haya ni mambo ya kawaida katika maisha kwani maisha ni mwigo, lakini mwigo wenye uhalisia wa kweli kulingana na mazingira, wakati, uwezo na uthubutu wa mtu katika jambo analolifanya.
Katika kufanikisha yale ambayo unayafanya na hata unayotaka kuyafanya kwa mafanikio, huna budi kufanya mambo kadha wa kadha kama tabia zako za kila siku za utendaji wako wa kazi.
Jaribu kufikiria juu ya uwezo ulionao katika utendaji kazi wako kwani wajasiriamali waliofanikiwa wanajua udhaifu wao na hawathubutu kuona kama vitu vya kuwakwamisha katika shughuli zao, bali wanachukulia kama moja ya fursa za kufikia malengo yao.
Wajasiriamali waliofanikiwa hujaribu kutumia njia mpya kwa lengo la kuimarisha mbinu za biashara zao kwa kuhakikisha kuwa hawafanyi upotevu wowote wa rasilimali katika mchakato mzima wa uendelezaji/uendeshaji biashara zao.
Jaribu kufikiria juu ya wateja wako kwani hao ndiyo roho ya biashara yako na bila wao hakuna biashara kwani hakuna familia yoyote hapa duniani ambayo imewahi kuendesha biashara kwa kujitegemea kama wateja wanaojitosheleza.
Jambo la msingi hapa ni kujua au kupata taarifa za jumla za idadi ya watu, hususani wateja ambao watakuwa watumiaji wa bidhaa au huduma unazozitoa kwani ni muhimu kukumbuka kuwa mchakato wa kutafuta soko au kujaribu kuuza bidhaa kwa watu ambao hawahitaji bidhaa/huduma husika ni jambo la kupoteza muda na kujitafutia matatizo yasiyo ya msingi kama vile msongo wa mawazo na kukata tamaa ya maisha.
Wajasiriamali waliofanikiwa hujikita zaidi kutafuta masoko kwa watu wanaohitajika au wanaohitaji bidhaa husika na hivyo kutumia muda vizuri na rasilimali zilizopo.
Pindi wajasiriamali wa aina hii wanapogundua kuwa wanakidhi mahitaji ya wateja wao hutafuta njia au mbinu za kuhakikisha kuwa wanawakamata na kuwakumbatia wasiwaponyoke.
Wajasiriamali hawa hufanya kila juhudi ya kuanzisha uhusiano mzuri wa muda mrefu kwani tunaambiwa kuwa mjasiriamali mzuri ni yule anayeona bidhaa yake kupitia mahitaji au dhima ya mteja wake.
Kufikiria juu ya biashara yako ikiwa ni pamoja na kufikiria kile kinachoendela nje ya biashara yako hasa kile kinachohusu au kinachoshabihana na biashara yako ili kuwa na uelewa mpana wa mambo mbalimbali yanayohusu shughuli unazozifanya.
Kufanya uchambuzi wa kina juu ya washindani wako wa biashara si tu kunakusaidia kujua unayeshindana naye bali pia kunakusadia kujua matatizo au makosa yanajitokeza katika biashara yako ikiwa ni pamoja na tafsiri ya kina juu ya biashara yako kwa lengo la kuleta ufanisi katika utendaji kazi wako.
Ingawa si vizuri kufikiria makosa au kuanguka kwako kulikotokea siku za nyuma ni vizuri pia ukatumia udhaifu au anguko la kipindi cha nyuma kama funzo la kuendesha mambo yako kwa mafanikio kwani wahenga wanasema binadamu hujifunza kutokana na makosa.
Mjasiriamali wa kweli haogopi kushindwa bali anafikiria zaidi namna ya kupata njia mbadala ya kurekebisha makosa yaliyotokana au yanayotokana na mchakato mzima wa shughuli za kijasiriamali kwa lengo la kupata mafanikio zaidi.
Mwandishi ni mtaalamu wa masuala ya
ujasiriamali
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!