Friday 5 December 2014

MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WANANCHI KUCHAGUA VIONGOZI WAADILIFU NA WENYE SIFA.


Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa Kata ya Ng’apa wilaya ya Lindi mjini kuchagua viongozi waadilifu na wenye sifa ambao watawaongoza wananchi kusimamia shughuli za maendeleo yao.


Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata hiyo.


Mama Kikwete alisema kuna baadhi ya watu wanachagua viongozi kwa ushabiki pasipo kuangalia kiongozi huyo kama ana sifa au la, na kuwasisitiza wananchi hao siku ya uchaguzi ikifika wasifuate mambo ya ushabiki na kuchagua kiongozi kwani ushabiki hauna manufaa yoyote.

“Nawaombeni muwapigie kura za ndiyo viongozi wote wa CCM wanaogombea nafasi za Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za Mitaa, kwani hawa wanasifa na mkiwachagua kutakuwa na manufaa kwenu na vizazi vyenu hivyo basi wote mliojiandikisha siku ya uchaguzi ikifika mjitokeze kupiga kura na kukichagua Chama chetu”, alisema .

Aidha MNEC huyo aliwakumbusha wanachama wa CCM siku ya uchaguzi kutokwenda kupiga kura wakiwa wamevaa sare za Chama au mavazi yoyote yenye kuonyesha ushabiki wa Chama cha siasa hiyo hairuhusiwi na kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Maadili ya vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi .


Kuhusu elimu Mama Kikwete alisema Serikali ya CCM kwa kushirikiana na wananchi imefanikiwa kujenga shule za Sekondari nchi nzima na ifikapo mwakani maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi katika shule hizo zitakuwa zimekamilika na kuanza kutumika.

Alisema, “Ninawaomba wazazi na walezi msimamie watoto waende shule ili wawe na maisha bora hapo baadaye kwani tatizo kubwa lililoko hapa ni watoto kutokwenda shule. Serikali imewajengea shule na maabara lakini kama watoto wenu hawataenda shule ni kazi bure, ili shule hizi ziwe na faida kwenu ni lazima watoto wenu wasome”.

Mama Kikwete pia alitembelea Kata ya Makonde na kuongea na wanachama pamoja na wagombea wa nafasi za Uenyeviti na Wajumbe na kuwapongeza viongozi wa zamani ambao wanamaliza kipindi chao cha uongozi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutekeleza na kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Aliwapongeza wanawake waliojitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi jambo ambalo litawawezesha kuingia katika ngazi ya maamuzi.

Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kichama ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye kampeni na kuwanadi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji utakaofanyika tarehe 14 mwezi huu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!