Thursday 11 December 2014

JK KUTOA MAAMUZI YA ESCROW WIKI IJAYO

Rais Jakaya Kikwete, anatarajia kutoa maamuzi kuhusiana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika 

akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wiki ijayo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kuwa Rais Kikwete atafanya maamuzi hayo baada ya kupokea ripoti, nyaraka na ushauri wa Bunge kuhusu akaunti hiyo. 

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Kikwete alipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na maazimio ya Bunge kuhusu akaunti hiyo. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya Rais kupokea nyaraka hizo, ameelekeza ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwa ajili ya umma kuisoma na kujua nini kimesemwa humo na kupendekezwa na CAG.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Rais Kikwete ameagiza pia ripoti hiyo itangazwe kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi nchini na mitandao ya kijamii ili isomwe na Watanzania wengi.

Taarifa iliongeza kwamba Rais Kikwete ameanza kupitia na kusoma nyaraka hizo na katika wiki moja ijayo, atazitolea maamuzi na kwamba yale mambo yanayomhusu moja kwa moja atayatolea maamuzi yeye, yale yanayohusu Serikali atayatolea maagizo na maelekezo ya namna ya kuyashughulikia.

Maamuzi yanayosubiriwa kwa hamu na wananchi wengi kufanywa na Rais Kikwete ni kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo; Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi; Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.

Mapendekezo ya kuwawajibisha viongozi hao yalitokana na maazimio ya Bunge Novemba 29, mwaka huu.

Juzi, Ikulu ilitoa taarifa kwamba Rais ameanza kazi rasmi baada ya kufanyiwa upasuaji nchini Marekani na afya yake kuimarika.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilieleza kwamba baada ya kuanza kazi, Rais Kikwete ataanza kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwamo kutoa maamuzi yaliyokuwa yanamsubiri.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!