Tuesday, 9 December 2014

HONGERA WATANZANIA KWA KUDUMISHA UHURU



TANZANIA Bara leo inaadhimisha miaka 53 tangu ipate uhuru wake kutoka katika makucha ya wakoloni Desemba 9, 1961.
Kwa vigezo vyovyote vile, kwa binadamu, umri huo ni wa utu uzima wenye kupitia mikikimikiki mbalimbali ya kimaisha bila kukata tamaa. Hongera sana Watanzania kwa kufikia umri huo mkiwa bado mnadumisha amani, upendo, umoja na mshikamano kama Taifa.


Tumefikia umri huu tukiwa tumebakiwa na mwaka mmoja kabla Serikali ya Awamu ya Nne, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba yetu.
Katika vipindi vya awamu zote nne za uongozi, taifa hili limepiga hatua mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Mambo machache ambayo tunaweza kukumbushana ni sekta ya elimu, ambapo sasa kila kijiji hapa nchini kina shule ya msingi huku kila kata ikiwa na sekondari yake.
Lakini, miaka ya mwanzoni mwa uhuru wetu wanafunzi waliokuwa wanachaguliwa kujiunga katika shule za sekondari, walikuwa ni wachache mno, kiasi kwamba wanakijiji walifurahia mtoto, hata kama ni mmoja tu, aliyechaguliwa kwenda sekondari ya serikali.
Furaha hiyo ilikuwa ni ya kijiji kizima. Kwa sasa hivi shule za sekondari zipo hadi ngazi ya kata, hivyo wananchi wengi katika kata wamejawa furaha.
Sambamba na shule za sekondari, idadi ya vyuo vikuu imeongezeka kutoka chuo kikuu kimoja cha Dar es Salaam hadi zaidi ya vyuo vikuu 20 hivi sasa, pamoja na vyuo vingine vya kati na vya ufundi vilivyosambaa nchini kote.
Kwa upande wa vyuo vikuu, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambacho bado kinaendelea kujengwa, kwa sasa kina wanafunzi 20,000. Wanafunzi wanaongezeka kila mwaka na ujenzi wake utakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wapatao 40,000.
Miundombinu ya barabara nayo haikusahauliwa. Kila baada ya muda fulani tunapata habari ya kuzinduliwa au kufunguliwa kwa ujenzi wa barabara nyingi za kiwango cha lami huku madaraja makubwa yakijengwa.
Mifano hai ni ujenzi unaoendelea wa daraja la Kigambo jijini Dar es Salaam na ujenzi mwingine wa daraja Kilombero mkoani Morogoro, ambao pia Rais aliuzindua Agosti mwaka huu katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Madaraja hayo mawili yanafuatia pia kukamilika kwa ujenzi wa daraja lingine kubwa la Malagarasi mkoani Rukwa. Ujenzi wa madaraja hayo, unakamilisha kiu ya serikali za awamu zote nne ya kupanga kujenga madaraja makubwa matano, mara baada ya kupata uhuru wetu.
Wakati awamu ya kwanza ilikamilisha ujenzi wa Daraja la Kirumu mkoani Mara, awamu ya tatu ilikamilisha ujenzi wa daraja lingine kubwa katika Mto Rufiji, maarufu kwa jina la Daraja la Mkapa.
Kwa upande wa siasa, Tanzania imepiga hatua, kama zilivyo nchi nyingine duniani, ambapo mwaka 1992 iliingia katika mfumo wa uchumi huria kutoka uchumi uliokuwa unadhibitiwa na serikali.
Lakini, pia iliingia katika mfumo wa vyama vingi kutoka mfumo wa chama kimoja. Tunapoadhimisha miaka 53 ya Uhuru, Tanzania ina vyama vya siasa vipatavyo 20 na mchanganyiko wa wabunge kutoka chama tawala na vyama vya upinzani vipatavyo vitano.
Katika kipindi hiki, pia Tanzania imeanza mchakato wa kupata Katiba Mpya. Mchakato huo umefikia kwenye hatua ya Katiba Inayopendekezwa.
Kinachosubiriwa sasa ni wakati mwafaka utakapofika, wananchi wataipigia kura Katiba hiyo, kwa maana ya kuikubali au kuikataa. Kwa ujumla, Tanzania imepiga hatua kubwa katika uhai wake kama Taifa. Mungu Ibariki Afrika. Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!