Wednesday, 17 December 2014

BASI LA MOHAMED TRANS WATANO WAPOTEZA MAISHA NA WENGINE 50 KUJERUHIWA VIBAYA




Watu watano wamekufa papo hapo na wengine 50 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Mohamed Trans walilokuwa wakisafiria kutoka jijini Mwanza kwenda Dar es salaam kupinduka katika kijiji cha Makomero, kata  ya Igunga, wilayani hapa, mkoa wa Tabora.



 Ajali hiyo ilitokea jana saa 5:30 asubuhi baada ya basi hilo lenye namba za usajili T 738 AAP kuacha njia na kupinduka mara nne.

Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo,  Maimuna Mussa  (27), aliyekuwa na mtoto wake,  Salima Athuman(2), alisema kuwa  alikuwa akitokea mkoani Mwanza kuelekea Dodoma.

Salima alisema kuwa walipofika katika kijiji cha Makomero  alishuhudia basi hilo likiacha njia na kupinduka mara nne. Alisema baadhi ya abiria walikuwa wakihaha kujinasua ili kuokoa maisha yao na wengine kunasa milango na madirishani.

“Kwa kweli Mungu ni mkubwa nimeshuhudia mwenyewe basi likipinduka mara nne lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mimi na mwanangu tumenusurika, tumetoka salama," alisema.
Aliwataka wamiliki wa mabasi kuwa na magari imara ambayo yanaweza kumudu safari za masafa marefu mbali na kudai kuwa  basi hilo linaonekana lina rangi nzuri lakini vyuma vyake vimechakaa siku nyingi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk. Fedilis Mabula, alilithibitishia NIPASHE kuwa wamepokea maiti watano, wakiwamo wanawake wawili na wanaume watatu.
Alisema pia wamepokea majeruhi  50 kati ya hao,  wanawake 23 na wanaume 27 na kwamba wamelazwa wodi namba nane ya Hospitali ya Wilaya ya Igunga huku hali zao zikiwa bado ni mbaya.

Kwa mujibu wa Dk. Mabula, maiti hao ambao wamehifadhiwa hospitalini hapo bado hawajatambuliwa.Naye Mkuu wa wilaya ya Igunga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo,  Elibariki Kingu, alisema chanzo cha ajali hiyo ni kukatika kwa usukani na kusababisha dereva kushindwa kulimudu basi hilo kisha kuacha njia na kupinduka.

Kingu alisema basi hilo huenda limepata ajali hiyo kutokana na uchakavu.Aliwashauri  wamiliki wa magari kuwa na uhakika na magari yenye uwezo wa kusafiri masafa marefu ili kuepusha ajali za mara kwa mara.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Suzan Kaganda, alisema Jeshi hilo bado linaendelea kufanya uchuguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo.

Kaganda aliwataka madereva hasa wa magari yanayobeba abiria kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha magari hayo kwa uangalifu mkubwa hasa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Krismas na mwaka mpya wa 2015.

“Taarifa za ajali hii nitatoa rasmi baada ya upelelezi wetu kukamilika,” alisisitiza Kamanda Kaganda.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!