Tuesday, 25 November 2014

WANAUME WATATU WAGOMBEA MAITI YA MWANAMKE



KATIKA hali isiyo ya kawaida, wanaume watatu, wawili wakazi wa jijini hapa na mmoja mkazi wa Nyamongo wilayani Tarime juzi wakiwa katika Mtaa wa Isagenge B, Kata ya Nyakato wilayani Nyamagana, walizua tafrani baada ya kung’ang’ania maiti ya Happy Wangoge Mathias (33) aliyekufa siku chache baada ya kuolewa na Paschal Mayala, jijini hapa.



Hiyo inatajwa ilikuwa ndoa ya tatu ya marehemu huyo anayedaiwa alikuwa ni mke wa mtu na kwamba aliolewa kwa mahari ya ng’ombe 11 na Chanjo Ryoba Wasinyo, mkazi wa Nyamongo, wilayani Tarime mkoani Mara aliyezaa naye mtoto wa kwanza wa kike (jina tunalo, ana umri wa miaka 14).
Vituko msibani
Tukio la kuing’ang’ania maiti hiyo lilianza rasmi Jumamosi iliyopita baada ya mke huyo kufariki dunia, ambapo inadaiwa wakati wa uhai wake, Happy akiwa anaishi jijini Mwanza akijihusisha na biashara ya samaki aliolewa na Benjamin Buchoti na baadaye hivi majuzi alifunga ndoa ya Kikristo na Mayala.
Aliyeanzisha vurugu hizo ni Buchoti ambaye alikuwa akiishi naye na kuzaa watoto wawili (majina na umri tunao), kabla mwanamke huyo hajafunga ndoa na Mayala hivi karibuni.
Buchoti uvumilivu ulimshinda baada ya kuwaelezea waombolezaji kuwa yeye ndiye mume halali wa marehemu kwa madai kuwa amezaa naye watoto wawili na alikuwa anaishi naye.
Alisema kutokana na ukaribu aliokuwa nao kwa marehemu mkewe na kuchuma naye mali pamoja, ikiwemo vyombo vya ndani, makochi, redio na vitu vingine, alidai kuwa watoto wasiende kumzika mama yao mpaka kwa kibali cha Mahakama kama njia ya kupata haki zake na watoto.
“Watoto wangu ni lazima wakapitie Mahakama ndipo waende wakamzike mama yao vinginevyo hawawezi kwenda kumzika mama yao”, alisema.
Kufuatia tukio hilo, watu kadhaa akiwemo Mwenyekiti wa Mtaa, Musa Ndaki walimtuliza Buchoti wakimsihi aache vurugu ili waangalie hoja iliyokuwa mbele ya kuandaa safari ya maziko ya kwenda kumzika marehemu.
“Kinachotakiwa hapa ni kuelewana na sio vurugu, tukio limekwishatokea hivyo lazima wote muafikiane juu ya jambo hili, vurugu kwa sasa hazina nafasi,” alisema Ndaki.
Baada ya ushauri huo, Buchoti alilegeza msimamo wa kung’ang’ania watoto wasiende kumzika mama yao, hivyo waliruhusiwa kupanda kwenye gari lililokuwa limebeba mwili wa marehemu kwenda kijiji cha Nyamongo kwa maziko, ingawa mtoto wa kiume (jina tunalo) alimkana mbele ya waombolezaji kuwa yeye si baba yake wa kumzaa.
Naye Mayalla anayedaiwa ni mume wa tatu aliyefunga ndoa na mwanamke huyo hivi karibuni na kubahatika kuishi naye kwa siku kumi tu kabla ya kuaga dunia, alizirai mara kadhaa msibani.
Aidha, alisema atakwenda kumzika marehemu nyumbani kwao Nyamongo wilayani Tarime. “Hata kama itakuwaje ni lazima niende nikamzike marehemu mke wangu”, alisema Mayalla msibani hapo.
Wakati hayo yakitokea, inaelezwa kuwa mume wa awali aliyemuoa mwanamke huyo ambaye inadaiwa alizuiliwa kijijini kwao Nyamongo asifike jijini Mwanza kwa kuhofia kuibua vurugu zaidi msibani, amedai wote wanaong’ang’ania maiti wanapoteza muda kwa madai kuwa Happy ni mkewe wa ndoa na alimtolea mahari.
Kwa mujibu wa mila za kabila la Wakurya, mke aliyeolewa na mume na akatolewa mahari, hata kama atakaa unyumba au kuishi na mume kabla hajavunja ndoa na mume aliyemuoa kwa kurudisha mahari, bado anahesabiwa ni mke wa mume wa kwanza aliyemuoa na watoto atakaowazaa nje ya ndoa nao ni halali.
Hoja ya Wasinyo iliungwa mkono na kaka wa marehemu, Matiko Mathias ambaye aliifuata maiti ya marehemu dada yake kuwa familia inamtambua mume halali ni Chanjo Waryoba Wasinyo ambaye alimtolea mahari marehemu dada yao.
“Sisi kama familia tunayemtambua ni Wasinyo ambaye ndiye mume halali aliyemtolea mahari dada yetu, wengine hao akiwemo huyo mpya walikuwa wapenzi tu”, alisema.
Aidha tukio hilo, lilisababisha chakula cha waombolezaji kutopikwa kwenye Nzengo (Mtaa) ambapo tukio hilo lilitokea.
HABARILEO hadi inaondoka msibani hapo ilishuhudia dagaa na maharage yaliyoandaliwa kwa ajili ya waombolezaji yakiwa kwenye sufuria bila kupikwa.
Aidha, mama mwenye nyumba alikokuwa amepanga marehemu, Monica Andrea alikabidhiwa kulinda nyumba ya marehemu na vitu vilivyomo, kwa madai kuwa vingeweza kuporwa na wanaodaiwa ni waume wa marehemu.
Inadaiwa Happy alianza kuugua siku mbili kabla ya sherehe ya kufunga ndoa yao, ambapo alilalamika kusumbuliwa na maradhi ya kichwa na kisha kulazwa kwa siku kumi katika Kituo cha Afya Buzuruga na siku ya 11 aliruhusiwa kutoka.
Taarifa zinadai, aliporudi nyumbani kesho yake alizidiwa tena na ndipo alipopelekwa kwa Mganga wa kienyeji wilayani Magu ambako alifariki dunia siku ya Jumamosi iliyopita majira ya asubuhi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!