Watu wanne wakiwamo askari polisi wamefariki dunia papo baada ya helkopta waliyokuwa wamepanda kuanguka eneo la Kipunguni B, Ukonga, jijini Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 4:00 asubuhi na watu waliofariki dunia wametajwa kuwa ni Kepteni SP Gidai Sindano, Inspekta Simba Muta, Rubani Joseph Alifayo kutoka maliasili na PC Josu Selestine.
Helkopta hiyo inamilikiwa na Wizara ya Mali Asili na Utalii.
Shuhuda wa tukio hilo, Beatrice Kamwela, ambaye sehemu ya duka lake limeharibika baada ya ajali hiyo, alisema wakati akiwa dukani alisikia mngurumo ulioambatana na kishindo kikubwa.
“Niliposikia mgurumo na kutazama nje nikaona helkopta inashuka ikagonga nguzo ya umeme na kuanguka, sehemu ya duka langu mbele imeharibiwa, nilikimbilia ndani maana niliwahi kusikia ndege inapodondoka hulipuka,” alisema.
Kamwela alisema eneo lilipoanguka helkopta hiyo mara nyingi watoto hupenda kucheza lakini wakati wa tukio hawakuwepo.
Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Hamisi Suleiman, alisema inawezekana waliokuwa kwenye chombo hicho walikuwa kwenye mafunzo au majaribio.
“Ndani ya helkopta kulikuwa na rubani mwandamizi na rubani wa kuifanyia marekebisho, ndio maana nasema inawezekana walikuwa kwenye mambo hayo mawili,” alisema.
Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku utaratibu wa kuyaondoa mabaki ya helkopta hiyo ukiendelea.
Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Flora Mwaikambo, alisema wakati inashuka kwenye anga matairi yake yalikuwa yameangalia juu.
“Inaelekea ilikuwa imepata hitilafu ikakosa mwelekeo, ilipoanguka ilijikusanya na kuwabana waliokowa mbele na nyuma, nilishuhudia mmoja aliyekuwa mbele mguu wake aliutoa nje, “ alisema na kuongeza:
“Baada ya tukio wananchi waliinyoosha na kutoa miili, wengine walitolewa nyama, waliharibika sana, gari la kubeba wagonjwa la hospitali ya Mselemu ilibeba miili hiyo,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment