Wednesday, 26 November 2014

WALIMU 826 NA WANAFUNZIWAO WAKIMBIA VITA KITETO

Siku kadhaa zimepita tangu kutokea kwa mapigano mapya kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.

Ni Alhamisi mchana, siku ambayo kwa kawaida ni ya masomo, lakini kimya kimetawala katika kijiji kizima cha Chekanao na Ilera huku sauti za ndege zikishamiri.
Makundi ya vijana na wakulima yanaonekana yakijadiliana na mbali yalipo makundi haya, vijana wa Kimasai nao wanaonekana wakiwa wametulia na fimbo zao.
Katika shule iliyopo kijijini hapo, polisi wametanda na silaha zao wakizungukazunguka. Anajitokeza mwalimu anayejitambulisha kwa jina la Paulo Sulle.
Akiwa bado na hofu anajitambulisha kuwa yeye ndiye mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi Chekanao.
Namuuliza kwa nini Alhamisi ambayo ni siku ya masomo, hakuna hata mwanafunzi mmoja darasani? Anajibu shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 526,lakini wote wamekimbia mapigano ya kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Anasema sambamba na wanafunzi pia walimu wenzake wanne waliokuwa wanaishi nje ya shule wametoweka. Amebaki yeye kwa kuwa anaishi katika nyumba iliyopo shuleni hapo.
‘’ Ililikuwa ni Novemba 13 jioni, kijiji kizima kilivamiwa na kundi la Wamasai zaidi ya 100 wakiwa na silaha mbalimbali siku moja baada ya kuuawa wenzao wawili na wakulima,” anasimulia.
Anaeleza kuwa wavamizi hao walipiga risasi kadhaa hewani na kuanza kupiga watu, kila mtu alikimbia kunusuru maisha yake.
Anasema baadhi ya wafugaji hao, walikaribia kufika shuleni na ndipo hofu ilitawala na wote kutawanyika tangu Novemba 13 na hadi Novemba 21 hakuna aliyekuwa amerejea.
Anasema kwa mazingira hayo, shule imejifunga yenyewe kwani hakuna amani na utulivu tena katika Kijiji cha Chekanao.
Mwalimu Paulo anasema kinachomsikitisha zaidi ni wanafunzi 80 wa darasa la nne ambao leo wanapaswa kufanya mtihani sasa haijulikani wapo wapi
“Tayari tumeletewa ratiba ya mitihani sasa watoto hawapo shuleni,” anasema kwa masikitiko.
Anafafanua kuwa hali hiyo ya kukosa amani imekuwa ikichangia shule hiyo kufanya vibaya kwani imekuwa kawaida sasa kila yanapotokea mapigano wanafunzi hukimbia na wengine kurejea baada ya mwezi mmoja hadi miwili.
“Oktoba 20 pia kulitokea mapigano huku, baada ya mkulima Abedi Muhogo kuuawa na hapo shule ilifungwa kwa wiki moja,” anasema.
Mwalimu mwingine, Pascalina Daffi anasema kukosekana amani katika vijiji vya wilaya hiyo, kunashusha ufaulu wa wanafunzi kila mwaka. “Ndiyo sababu utaona mwaka huu kati ya watoto 37 amefaulu mmoja tu na mwaka 2013 kati ya watoto 36 waliohitimu la saba amefaulu mmoja tu, ” anasema.
Anatoa wito kwa Serikali kujitahidi kusaka amani Kiteto kwani madhara yake ni makubwa.

Shule ya Ilera
Kama ilivyo Chekanao, takriban kilomita tano kutoka hapo, ipo shule nyingine ya Ilera. Kwa msaada wa askari nimefika hapo na kuikuta shule nyeupe.
Nikiwa hapo nakutana na mwanakijiji aitwaye Daniel Lemaya anayejitambulisha kuwa ni mjumbe wa kamati ya shule. Anasema walimu na wanafunzi wamekimbia.
“Hali ni mbaya vita hii ina athari kubwa sasa tunanyima elimu hawa watoto ambao ni taifa la kesho,” anasema.
Anasema kuwa tangu Novemba 13 hadi Novemba 21 hakuna mwalimu wala mwanafunzi aliyefika shuleni wote wapo vichakani na nje ya kijiji hicho.
Hata hivyo, ananipa namba ya simu ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Kolneli Akwezo ambaye baada ya kuwasiliana naye anakiri kuwa wanafunzi wake 300 hawajulikani walipo na pia walimu.
“Mimi mwenyewe sipo shuleni hakuna mwanafunzi hata mmoja na walimu wangu wote sita wameshindwa kurejea shule wakihofu mapigano hayo kutokea tena, ”anasema na kuongeza:
“Shida kubwa hakuna amani na pia walimu tunaishi mbali, safari ya kutoka nyumbani hadi shuleni lazima upite uwanja wa mapigano.’’ Anasema kibaya zaidi mapigano hayo, yamekuwa yakisababisha maafa kwa watu wasio na hatia

Viongozi wazungumza
Mwenyekiti wa kitongoji cha Changanyikeni kilipo kijiji cha Chekanao, Abubakar Nchii anakiri kuwa wanafunzi na wazazi wao wamekimbia vita.
“Watu wamekimbilia Wilaya za Kondoa, Kongwa na wengine wamekwenda vijiji vingine vya Kiteto kuhofia vita, sasa lazima shule zikose wanafunzi,” alisema.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Kiteto, Boscal Ndunguru alikiri shule kuathirika na mapigano na kueleza kuwa timu ya kitaifa ipo Kiteto kupata suluhu ya mapigano hayo.
“Ni kweli tuna taarifa ya shule kuathiriwa na mapigano haya na jitihada za kuleta amani na utulivu zinaendelea na tunadhani hali itarejea kuwa ya amani na shule kuendelea,” anasema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Deusdedit Nsimike anasema: ”Ni kweli kuna shule zimeathirika lakini tunawaomba wazazi na walimu kurejea katika makazi yao, kwani hali ni shwari polisi wapo maeneo yote yenye migogoro.”
Haya ni sehemu tu ya madhara ya mapigano kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto. Mapigano haya yasipopatiwa ufumbuzi, wanaoathirika ni wengi wakiwamo watoto wanaokosa elimu ambayo ndiyo mkombozi wa maisha yao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!