Wednesday, 26 November 2014
TUIMARISHE MSAKO DHIDI YA MAUAJI YA WANAWAKE
VYOMBO vya habari jana viliripoti taarifa ya kuwepo kwa wanaume wawili jijini Dar es Salaam, wanaowarubuni wasichana na wanawake kwa ujumla kufanya nao mapenzi na kisha kuwaua.
Vyombo vya habari vilikuwa vinamnukuu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ambaye alisema tayari wanawake sita jijini Dar es Salaam wameshakumbwa na njama za majahili hao na kisha kuuawa.
Tunapenda kuunga mkono tahadhari iliyotolewa na Kamanda Kova kwa wanawake wote kutokubali kushawishiwa kirahisi na wanaume wasiowajua kwa lengo la kufanya nao mapenzi, kutokana na ukweli kwamba wanaweza kutumbukia katika mitego ya majahili hao, ambao bado hawajatiwa mbaroni.
Katika hili ni vyema wanawake kwa wanaume, viongozi na wasio viongozi kushikamana kwa kila hali katika harakati za kuwafichua mafedhuli hao popote walipo ili wasituvurugie amani na utulivu unaotamalaki katika nchi yetu.
Hili siyo jambo dogo na bila shaka wahalifu hao, wanatumia mbinu za aina yake katika kufanikisha mawindo yao, lakini tunachosema ni kwamba kila inapobainika kuwepo na wasiwasi wa watu wa aina hiyo ni vyema wakaripotiwa kwenye vyombo vya usalama vikiwemo polisi.
Tunasema hivi kwa sababu ni vigumu, kuwatambua kwa urahisi watu kama hao, kwa kuwa kwa mujibu wa maelezo ya Kova mbinu wanazotumia ni pamoja na kuwapatia huduma mbalimbali za kimaisha na kisha huishia kuwaua.
Ndiyo maana tunasema wanawake waongeze umakini wao katika mahusiano ya kijamii, kwani wanaweza kutumbukia katika mtego wa watu hao.
Hapa tunapenda kukumbushana tu baadhi ya mambo ya msingi katika kuingia katika uhusiano, ikiwa ni pamoja na kumjua angalau ni nani unayehusiana naye, ikiwa ni pamoja na majina yake, anafanya shughuli gani jijini, kwao ni wapi na hata nyumbani kwake kwa maana ya mkoa anaotoka ili angalau kujiridhisha tu kwanza kabla ya kujitumbukiza moja kwa moja.
Tufahamu pia kwamba kwa kutaka kujua hayo yote kuna faida, lakini pia watu hao wanaweza kutumia mbinu ya kumwaga fedha, hivyo mhusika kujisahau katika kupata taarifa za msingi na kuishia kwenye kifo mikononi mwa watu hao hatari ndani ya jamii yetu.
Hebu tuanze kwa makusudi mtindo mpya wa kujuana kabla ya mambo yote ya mahusiano, kujiridhisha na masuala ya usalama kwanza. Tukiukaribisha utamaduni wa aina hii unaweza kutuvusha katika janga hili, ambalo tayari limo ndani ya jamii yetu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment