Tuesday, 25 November 2014

POLISI YAONYA WANAWAKE KUJICHUNGA NA WAUAJI DAR

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

KUTOKANA na kushamiri kwa matukio ya wanawake kuuawa na watu wanaodhaniwa ni wapenzi wao wa muda mfupi, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewaonya wanawake jijini Dar es Salaam kuwa makini na baadhi ya wanaume wanaowataka kimapenzi na kuwaua kisha kutelekeza miili yao.



Aidha, imeelezwa kuwa katika siku za hivi karibuni yameripotiwa matukio kadhaa ya mauaji ya aina hiyo, ambapo kwa sasa wanawake sita tayari wamepoteza maisha.
Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova kwa vyombo vya habari, akiwataka wanawake kuchukua tahadhari juu ya wanaume wanaowataka kimapenzi kwa kuwa kuna uwezekano wa kuhatarisha maisha yao au ya familia zao.
Kumekuwepo na taarifa juu ya kuwepo kwa wanaume wawili, wanaowashawishi wanawake kuwa nao kimapenzi na baada ya muda huwaua.
“Inaaminika watu hao huwashawishi akina dada au wanawake kwa jumla ili wawe nao kimapenzi huku wakiwasaidia kwa huduma mbalimbali za kimaisha na kisha kuwaua,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kova alitoa wito kwa wanawake wote, kutokukubali kushawishiwa kirahisi na wanaume wasiowajua, ambao wanataka kuwa nao kimapenzi, kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kuingia katika mtego mbaya na pengine hata kuyaweka maisha yao rehani.
Aidha, Kova alisema katika siku za hivi karibuni, yameripotiwa matukio kadhaa ya mauaji ya aina hiyo, ambapo kwa sasa wanawake sita tayari wamepoteza maisha.
Hata hivyo madhumuni ya wauaji hao hayajafahamika, ila inawezekana mauaji hayo yakahusiana na mambo ya ushirikina.
Kova alitaka wakazi wa jiji hilo, kutoa taarifa sahihi kwa polisi na vyombo vingine vya usalama ili kuwabaini wahalifu hao na kuwakamata ili sheria ichukue mkondo wake

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!