Spika wa Bunge, Anne Makinda amewataka wabunge kujadili ripoti ya Escrow bila kuingiza hisia za uchaguzi mkuu ujao na ushabiki wa wagombea kwa kuwa rais ajaye Mungu pekee ndiye anayemjua.
Akizungumza kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo bungeni jana, Makinda alisema, “Tatizo lenu ninyi ndiyo mnaovunja kanuni maana mnaacha facts (hoja) na kuanza kujadili masuala yasiyohusiana, hapa naomba mzingatie kuwa TBC inaonekana dunia nzima, hivyo watu wanawaangalia,” alisema Makinda.
Aliwataka wasitumie nafasi hiyo pia kulipizana visasi ikiwamo kutokutumia nafasi hiyo kupiga kampeni na blabla za mwaka 2015.
“Niwaambie kuwa rais ajaye Mungu ndiye anayemjua na tayari ameshaandaliwa, sasa hakuna haja ya kuchafuana kutokana na suala hilo,” alisema Makinda na kushangiliwa na wabunge wa pande zote.
Alisema wamepokea barua ya mahakama kuhusu mjadala huo, lakini ilikuwa ya mashaka kwani iliandikwa saa 8:00 mchana wakati kesi ilisomwa saa 8:30 mchana hivyo ripoti ya Escrow lazima ijadiliwe.
Mapema, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro alitoa ufafanuzi wa amri iliyotolewa na Mahakama Kuu juzi.
“Jana Bunge lilipokea barua ya zuio kutoka mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikilitaka Bunge lako kutoendelea na mjadala au kufanya chochote kitakachoibua mjadala katika ukaguzi maalumu katika Akaunti ya Tegeta Escrow,” alisema Dk Migiro.
Alisema kuwa shauri hilo namba 51/2014, lilikuwa ni kutaka Bunge lisijadili suala hilo hadi maombi ya msingi yatakaposikilizwa.
“Kupitia mjadala ulioibuliwa leo asubuhi ndani ya Bunge lako na ningependa kufanya rejea katika ibara ya 100 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (Kutakuwa na Uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautajadiliwa mahali popote au kuhojiwa na chombo chochote).
Alisema kuwa majukumu ya mahakama yameainishwa katika ibara ya 100(a) ambayo inasema kuwa mahakama kitakuwa ndicho chombo cha mwisho kwa utoaji haki kwa shauri lolote.
Alisema uamuzi uliotokea mahakamni ulikuwa ni kutaka mambo yabaki kama yalivyo (status quo).
Alifafanua kuwa, uamuzi huo ulikuwa na maana kuwa Bunge linaweza kuendelea na vikao vyake na ratiba kama ilivyokuwa imepangwa (status quo) ikiwamo uwasilishaji wa taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa PAC.
Wakati wote alipokuwa akisoma taarifa hiyo, wabunge wengi walionekana kutomwelewa na mara zote walikaa kimya wakitaka kujua kinachoendelea, lakini alipohitimisha alishangiliwa.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment