Unaposikia au kuona maziwa ya mtindi, hisia zinazokufikia haraka ni zile za uchachu na ladha nzuri ya kinywaji hicho.
Lakini utafiti mpya umethibitisha kuwa mtindi ni zaidi ya kinywaji, ni tiba ambayo inakuokoa na maradhi yasababishwayo na mazingira yetu.
Utafiti uliofanywa nchini na Taasisi ya Microbiology ya Marekani na kuchapishwa katika jarida la The Science Daily umeeleza kuwa maziwa ya mtindi yana bakteria rafiki ambao wana uwezo wa kuwalinda watoto na wajawazito na kemikali nzito za sumu.
Madaktari wa Kitanzania kwa kushirikiana na wale wa Canada walitengeneza maziwa ya mtindi yenye bakteria hao aina ya Lactobaciluus Rhamnosus kisha kuyagawa kwa wahusika ili kupata matokeo.
Wakiongozwa na Dk Gregor Reid, watafiti hao walibaini kuwa bakteria hao wana uwezo wa kumkinga mtu na mazingira yanayohatarisha afya katika maeneo duni duniani.
“Tulibaini kuwa metali na kemikali zenye sumu zinazuiwa kuingia kwenye mwili wa binadamu hasa wakati wa kula iwapo mtu atatumia maziwa ya mtindi,” ilisema sehemu ya utafiti huo.
Akifanya kazi na Taasisi ya Western Heads East, Dk Reid ameanzisha mpango wa kutengeneza bakteria hao katika baadhi ya jamii mkoani Mwanza.
Nia ni kuanza kuusaidia mkoa huo ambao upo katika Ziwa Victoria ambalo limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na dawa za kuua wadudu na sumu nyingine za metali pamoja na zebaki.
Akielezea manufaa ya maziwa ya mtindi kwa afya, Mtaalamu wa Chakula na Lishe kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Pazi Mwinyimvua anasema kuwa, uchakataji wa mtindi huendana na bakteria wazuri ambao ni kinga tosha mwilini ya baadhi ya magonjwa.
Mwinyimvua anabainisha kuwa uchachu uliopo unatokana na vunjavunja ya maziwa na kupatikana mtindi ambapo hali hiyo ndiyo huleta faida nyingi.
“Kwa mfano unapokula chungwa moja unapata faida ndogo tofauti na unapokunywa bilauri moja ya juisi yake kwa kuwa inakuwa imeshasagwa na kuchujwa, ni sawa na mtindi ule utaratibu wa kuhama kutoka katika maziwa ya kawaida na kuwa mtindi, ndiyo unaoongeza vitamini na faida ya kujikinga na maradhi mbalimbali,” anasema Pazi.
Dk Badru Mustapha anavitaja virutubisho vinavyopatikana kwenye mtindi kuwa ni pamoja na ‘Calcium’, ‘Phosphorus’, ‘Riboflavin (vitamin B2), ‘Iodine’, ‘vitamin B12’, ‘Pantothenic acid (vitamin B5) ‘Zinc’, ‘Potassium’ na ‘Molybdenum’ ambavyo ni kinga tosha mwilini
Anafafanua tofauti iliyopo kati ya maziwa ya kawaida na mtindi kuwa ni kuwapo kwa ‘bakteria hai’ ambao ni nadra sana kuwapata katika chakula au kinywaji kingine.
Anasema bakteria hao wakiwa kwenye chakula kingine wanakifanya kuchacha badala ya kukipa faida na ubora kama ambavyo hufanyika kwenye mtindi.
Huongeza siku za kuishi
Kauli za wataalamu hao kutoka Tanzania zinaungwa mkono na wataalamu kutoka nje ambao wamebainisha hayo kupitia utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Cha Canadian kupitia kitengo cha ‘Centre for Human Microbiome and Probiotics’, na kuongozwa na Dk Gregor Reid.
Utafiti huo unaonyesha kuwa unywaji wa mtindi mara kwa mara, hasa katika kundi la wazee, huupa mwili uwezo wa kupambana na magonjwa mbalimbali. Utafiti huo umeonyesha kuwa maziwa yanausaidia mfumo wa kinga ya mwili kuwa imara zaidi.
Reid anasema wakati wa kufanya utafiti huo alichukua, wazee 162 waliopewa utaratibu wa kunywa mtindi na maziwa zaidi ya mara tatu kwa wiki na kufuatiliwa maendeleo yao kwa muda wa miaka mitano.
“Matokeo yalionyesha kuwa idadi ya vifo vya wazee hao ilipungua kwa asilimia 38 ukilinganisha na kundi la wazee wasiotumia au waliotumia mtindi kiasi kidogo sana, ”anasema Dk Reid.
Utafiti uliochapishwa katika kitabu kiitwacho “Mayo Clinic Book of Home Remedies” uliosimamiwa na Dk Philip Hagen katika hatua zote yaani utafiti na uchapaji, ilionyesha kuwa unywaji wa mtindi hupunguza maambukizi ya maradhi ya ukeni.
Dk Hagen katika kitabu hicho alibainisha kuwa mtindi, umeonesha kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa kinga dhidi ya maambukizi ya ukeni.
Anafafanua kuwa katika utafiti huo walihusisha wanawake wenye magonjwa ya kuambukiza sehemu za siri, baada ya kutumia mtindi kiasi cha paketi moja kila siku kwa muda wa miezi sita, maambukizo hayo yalitoweka.
Licha ya kinywaji hicho kuonekana kizito wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Marekani kiitwacho ‘American College of Nutrition’ (ACN) wamesema kuwa tafiti zinaonyesha mtindi pia hupunguza mafuta mwilini na kwa maana hiyo una uwezo wa kupunguza unene.
Kadhalika utafiti huo umesisitiza na kutoa angalizo kuwapo na matumizi sahihi ya kinywaji hiki hususani kuzingatia unywaji wa mtindi halisi uliotengenezwa kutokana na maziwa halisi ya ng’ombe, kwa sababu siri kubwa iliyomo kwenye mtindi ni ule uchachu unaotokana na ‘bakteria hai’ wanaopatikana baada ya maziwa kuganda na kuchachuka
No comments:
Post a Comment