Idadi kubwa ya watu wamefanya maandamano mapya kuhusu uamuzi wa mahakama kutomfungulia mashitaka polisi mzungu aliyemuua kijana mwafrika mweusi katika mji wa Ferguson, Missouri.
Maandamano hayo yaliyofanyika kuanzia mjini New York hadi Seattle yalikuwa ya amani ingawa vurugu zilizuka mjini Oakland, California na katika miji mingine 13.
Kulikuwa na ghasia pia katika mji wa Ferguson huku polisi wakiwakamata watu 44 ingawa uharibifu mkubwa ulifanyika zaidi Jumatatu.
Afisa aliyemuua kijana Michael Brown anasema hakuwa na nia mbaya bali alikuwa anatekeleza majukumu yake kama mlinzi wa umma.
Afisaa huyo, Darren Wilson, aliyempiga risasi Michael aliyekuwa na umri wa miaka 18, aliambia, shirika la habari la ABC, kwamba wakati alipokuwa anapambana na kijana huyo kabla ya kumuua alihisi kama aliyekuwa anapimana nguvu na Hulk Hogan.
Afisa Darren aliambia mahakama kuwa anajua kuwa alifanya kazi yake vyema.
Watu wengi katika mtaa wa Ferguson ambao wenyeji wake wengi ni waafrika weusi, walitaka afisa huyo ashitakiwe kwa kosa la mauaji lakini uamuzi wa mahakama ulifikia kuwa polisi huyo hatakabiliwa na kosa lolote kwa mauaji ya Michael.
Mawakili wa familia ya Brown waliuponda sana uamuzi wa mahakama wakisema haukubaliki kamwe na wala sio wa haki.
Magari ya polisi yalishambuliwa katika maandano yaliyozuka baadaye huku polisi wakilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao katika mji wa Ferguson wenye idadi ya watu 21,000 .
No comments:
Post a Comment