Sunday, 30 November 2014

KUWA MAKINI DAWA HIZI ZISIWE SUGU KWA VIMELEA WA MALARIA

Mwishoni mwa mwaka jana taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zilionyesha kuwa Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano, vinavyotokana na ugonjwa wa malaria.


Pamoja na mafanikio hayo yote bado malaria ni ugonjwa tishio nchini na duniani kwa jumla, hasa kwa nchi zilizopo ukanda wa kitropiki. Hapa Tanzania, kila mwaka karibu watu 60,000 hadi 100,000 hufariki dunia kutokana na ya ugonjwa huo.

Matibabu ya malaria yamekuwa na changamoto nyingi sana kwa upande wa dawa, vipimo, madhara ya ugonjwa, namna ya kuudhibiti, kujikinga na mabadiliko ya vimelea vya ugonjwa huo.
Tayari kuna taarifa iliyotoka hivi karibuni katika mtandao wa WHO kuwa kwa nchi ya Thailand na Cambodia kwamba umetokea usugu wa dawa mseto kwa kiambata kimojawapo cha artemesenin. Nchi hizi kimazingira zinafanana na Tanzania na kwa upande mwingine sababu za kujitokeza kwa usugu wa dawa ni kama zinazotokea hapa kwetu.

Nakumbuka ulitokea usugu ka wa dawa ya Klorokwini na baadaye ASP. Kwa sasa Alu ndiyo dawa madhubuti zaidi kutibu malaria na inapatikana kwa bei nafuu.
Tabia zetu ni moja ya mambo yanayochangia kutokea kwa usugu wa dawa. Tabia hizo ni za kutumia dawa bila ya ushauri wa wataalamu wa afya na kutomaliza dozi husika kama inavyotakiwa.

Sababu nyingine inayochangia tatizo hili ni uwepo wa dawa bandia au dawa zilizo chini ya kiwango. Tanzania inapakana na nchini nane na ni vigumu kudhibiti uingizwaji wa dawa kutokakana na wengine kuziingiza kwa njia ya panya.
Wagonjwa wanatumia dawa moja kama vile SP, chlorokwini na metakelfini. Mwongozo wa matibabu ya WHO unaonyesha kuwa dawa mseto ni muunganiko wa dawa zaidi ya mbili.
SP imebaki kama kingatiba kwa wajawazito ambao ni kundi dogo sana katika jamii, hivyo kutokuwa na athari katika eneo hili.
Tayari tafiti mbalimbali duniani kupitia Shirika la Afya Duniani zimeonyesha kuwa dawa moja haiwezi kutibu malaria.

Ingawa pia zipo dawa mseto za aina nyingine tayari kuna watafiti hapa nchini waliogundua kuwa mchanganyiko huo haufai kutumika kwa Watanzania.
Changamoto nyingine ni malaria kuwa na dalili zinazofana na magonjwa mengine hivyo mhudumu wa afya asiye na uzoefu au uangalifu huweza kuchukua uamuzi wa harakaharaka kuwa ni malaria.

Elimu ya sayansi ya tiba inaonyesha kuwa ugunduzi wa tatizo alilonalo mgonjwa ni umakini wa vipimo na historia ya mgonjwa.
Hata hivyo, uzoefu na ujuzi wa mhudumu ndiyo nyenzo ya kumfanya mhudumu wa afya kugundua ugonjwa kwa asilimia 80. Asilimia 20 hutegemea vipimo vya maabara.

Mfano mzuri ni zahanati zilizo pembezoni mwa nchi ambako hazina maabara za uchunguzi na kuna mhudumu mmoja tena ni muuguzi. Hakuna daktari wala maabara. Bado jamii yetu haijaelimika vya kutosha juu ya umuhimu wa kutumia dawa kwa usahihi. Wengi huishia njiani wanapopata nafuu. Ni moja ya sababu ya kuchangia usugu wa dawa za malaria.

Hivyo ni muhimu Watanzania tuwe makini na mambo haya yanayoweza kuepukwa mapema ili tusije tukawa kama Thailand na Cambodia.

Nchi yetu ina wataalamu wa afya, watafiti, madaktari bingwa hivyo wanapaswa kutumiwa katika ushauri ili kuiokoa nchi kwenye janga la usugu wa dawa ya Alu.

Jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele kuepuka kutumia dawa za malaria bila ushauri wa wataalam afya.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!