Friday, 28 November 2014
BUNGE LAELEZWA MAGUNIA YALIVYOBEBA FEDHA IPTL
WATU mbalimbali na viongozi wa umma waliofaidika na fedha za akaunti ya Tegeta Escrow ya Kampuni ya kufua umeme ya IPTL, wametakiwa kurejesha fedha hizo, kufilisiwa mali zao na kushitakiwa mahakamani.
Aidha, mmiliki wa Kampuni ya PAP, Harbinder Singh Sethi ameamriwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha haramu, ukwepaji wa kodi na wizi.
Pia kwa kutumia sheria za nchi, kuhakikisha Sethi anarejesha fedha zote alizochota Benki Kuu ya Tanzania, na kwamba kwa suala la utakatishaji wa fedha haramu, mamlaka ziwasiliane na nchi nyingine kuhakikisha mali za Sethi zinakamatwa na kufidia fedha hizo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imependekeza hayo jana wakati ilipowasilisha bungeni mapendekezo yake kutokana na matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akisoma mapendekezo maoni na mapendekezo ya Kamati baada ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe kusoma sehemu ya uchambuzi wa sakata hilo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema Kamati inazitaka mamlaka za uchunguzi kuhakikisha kuwa fedha hizo zinarudi Benki Kuu hata kama ikibidi kufilisi mali za watu wote waliofaidika na fedha hizo thamani ya fedha walizopewa na James Rugemalira, mmoja wa wanahisa wa IPTL kupitia kampuni yake ya VIP Engineering.
“Kwa mujibu wa taarifa ya CAG na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu mbalimbali binafsi. Kamati haina tatizo na watu wawili kuuziana makampuni yao kwa thamani wajuazo wenyewe, au jinsi ya kuzitumia fedha zao, ama kuwachagulia watu wa kuwagawia, lakini Kamati imejidhihirishia kuwa sehemu iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu,” alisema Filikunjombe.
Kamati hiyo ilisema Rugemalira aliuza hisa zake za VIP kwa Sethi kutoka katika fedha za Tegeta Escrow, na kuthibitisha kuwa fedha hizo zililipwa katika Benki ya Mkombozi Commercial Bank ambako ziligawawiwa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa umma, wanasiasa, watendaji wa mashirika ya umma, watumishi wa umma, majaji na viongozi wa dini.
Zitto katika taarifa yake aliwataja viongozi wa kisiasa ambao waliingiziwa fedha zao katika akaunti binafs ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa zamani na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Sh bilioni 1.6, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuika, Sh bilioni 1.6, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Daniel Yona waziri mwingine wa zamani wa wizara hiyo na mbunge mstaafu Paul Kimiti kila mmoja alipewa Sh. milioni 40.4 huku Dk Enos Bukuku aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Tanesco aligawiwa Sh. milioni 101.7.
Kwa majaji, aliwataja Profesa Eudes Ruhangisa na Jaji J. Mujulizi ambao mmoja alilipwa Sh milioni 404 na miwingine Sh milioni 40.4. Kwa upande wa watumishi wa umma ni Philip Saliboko aliyekuwa RITA na Emmanuel Ole Naiko aliyekuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kila mmmoja alipata Sh milioni 40.4 na Lucy Apollo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ni Sh milioni 80.8.
Kwa upande wa madhehebu ya dini, Zitto aliwataja Askofu Method Kilaini million 80.8 Askofu Eusebius Nzigilwa Sh milioni 40.4 na Mchungaji Alphonce Ye Simon alipata Sh milioni 40.4.
Zitto alisema baadhi ya watu hao walienda kugawana fedha benki tajwa wakiwa na mifuko ya Rambo, sandarusi, maboksi, magunia na lumbesa.
Benki ya Mkombozi inamilikiwa na Kanisa Katoliki Tanzania. Kuhusu watu hao, Filikunjombe alisema baadhi ya waliofaidika na fedha hizo ni viongozi wa umma ambao wanapaswa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayowataka kutoa taaria ya zawadi mbalimbali wanazopokea au malipo wanayolipwa.
“Vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi kutambua kama walifuata matakwa ya sheria na hatua mahsusi zichukuliwe ikiwemo kuvuliwa nyadhifa zao zote za kuchaguliwa na/au kuteuliwa, kufilisiwa mali zao na kushitakiwa mahakamani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 132 (1) – (6),” alisema.
Pia fedha zilizolipwa kwa PAP ambayo si mmiliki halali wa IPTL kwa maana hiyo fedha hizo zilitolewa kwa watu hao kama rushwa na kutakatisha fedha hizo haramu.
Kamati ilipendekeza kwamba akaunti zote zilizohusika na miamala haframu ya akaunti ya Tegeta Escrow, akaunti zao zifungwe (freeze) na wenye akaunti hizo walazimishwe kuzirejesha fedha hizo kwa mujibu wa sheria ya Anti Money Laundering pamoja na mali zao kufilisiwa.
Aidha, Kamati imetaka kuvunjwa mara moja kwa Bodi ya Tanesco na Takukuru iwafungulie mashtaka ta matumizi mabaya ya ofisi wajumbe wote waliohusika kupitisha maamuzi hayo ya kifisadi ili iwe fundisho kwa wajumbe wengine wa Bodi za mashirika ya umma kwamba watahukumiwa kwa maamuzi mabovu wanayoyafanya.
HABARI LEO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment