Thursday, 23 October 2014

WANAUME WASHUHUDIE WAKE ZAO WAKIJIFUNGUA

DHANA ya kutaka wanaume kushuhudia wake zao wakijifungua hospitalini, imeonekana kutokubalika kirahisi miongoni mwa jamii kutokana na kile kinachodaiwa kuwa mila na desturi nyingi hazitoi baraka juu ya hilo.


Katika mkutano kati ya Shirika la Muungano wa Utepe Mweupe na Uzazi Salama Tanzania ulioshirikisha wadau wa afya katika Kata ya Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga, jana mjini hapa, baadhi ya wachangiaji wamesema panahitajika mabadiliko ya taratibu kwa jamii kukubaliana na hilo.
Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe, Rose Mlay, katika mazungumzo juu ya mikakati ya kukomesha vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, pamoja na masuala mengine, alishauri wanaume wasiishie kusindikiza wake zao kliniki, bali pia washuhudie wanavyojifungua.
Mkutano huo ulifanyika katika Kituo cha Afya cha Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga ambako watendaji wa shirika hilo walitembelea kupata maoni ya jamii na mamlaka juu ya mkakati wa kupambana na vifo vya mama na mtoto chini ya kampeni yake ya ‘Wajibika Mama Aishi’. Diwani wa Kata ya Mazwi, Joseph Ngua alisema suala hilo linahitaji uelimishaji wa kina kwa wanaume.
“Kinachotawala zaidi ni mila na desturi. Hatukuzoea baba kushuhudia mke anavyojifungua. Lakini kwa sasa kumpeleka mama kliniki halina mjadala, lakini kwenda chumba cha kujifungulia, ni gumu mno.”
Naye Mtendaji wa Kata ya Mazwi, Justus Athanas alisema kama suala ni mume kushuhudia uchungu anaopata mkewe ili asimzalishe watoto wengi, pia upande wa wanawake wanapaswa waulizwe wanapokubali kuendelea kuzaa wanakuwa wamesahau uchungu.
“Kama baba anashauriwa kuingia ashuhudie uchungu anaopata mke, je akinamama nao wanakumbukumbu na uchungu? Mwingine ukimwambia tupange idadi ya watoto ataanza kuleta wivu, atasema umepata mwanamke mwingine,” alisema.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mazwi, Dk Elinjikanyia Moshi , alikiri wanaume kutoruhusiwa kuingia chumba cha kujifungulia. Hata hivyo alisema, kadri uelimishaji unavyoendelea ikiwamo kuhamasisha wanaume kupeleka wake zao kliniki, pia suala hilo baadaye linawezekana.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!