Monday, 20 October 2014
RAIS KABILA AMSHUKURU RAIS KIKWETE
RAIS Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania.
Aidha amemuomba Rais Kikwete kuendelea kuhakikisha kwamba uhusiano unaendelea kudumu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Kabila alizungumza hayo baada ya Rais Kikwete kuwatunuku Kamisheni ya Luteni usu wanafunzi 437, wa Tanzania na wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, chuoni Monduli jana.
Katika maofisa hao ambao wamehitimu mafunzo ya kijeshi katika Chuo cha maofisa wa jeshi kilichopo Monduli mkoani Arusha, wanafunzi 23 ni Watanzania na wanafunzi 414 wa Kongo, ambao watatunukiwa uofisa pindi watakaporejea nchini kwao.
Kwenye hafla hiyo, Rais Kabila alipata fursa ya kuwakabidhi zawadi wanafunzi watatu ambao wawili kutoka DRC Kongo na mmoja Tanzania ambao wamefanya vizuri katika mafunzo hayo.
Hii si mara ya kwanza kwa DRC Congo, kupeleka maofisa wake kwenye chuo hicho cha mafunzo ya maofisa wa kijeshi cha Monduli.
Aidha amesema maofisa hao watasaidia kuongoza mapambano dhidi ya maadui waliopo nchini humo, ambao wanarudisha nyuma maendeleo ya wananchi wa nchi hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Msemaji wa Jeshi, Meja Joseph Masanja, akizungumza na waandishi wa habari kabla ya wanafunzi hao kutunukiwa kamisheni, amesema kuwa Tanzania ni kituo kikubwa cha kufundisha maofisa wa jeshi wa mataifa ya ukanda wa Maziwa Makuu.
Amesema nchi ya Kongo na Tanzania ni marafiki na lengo la kutoa mafunzo hayo kuleta amani katika nchi hiyo.
Amesema kuwa amani inaletwa na majeshi yenye nidhamu hivyo hao watakaporudi kwao itakuwa chachu ya kupatikana kwa amani nchini humo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment