Mwanamama Neema Iwena aliyekatwa mapanga na mumuwe, Victor Nzali. Kwa mujibu wa mashuhuda wetu, tukio hilo la kutisha, kusikitisha na la ukatili wa kijinsia lilijiri nyumbani kwa wanandoa hao katika Kijiji cha Mlimba, Ifakara mkoani Morogoro na kusababisha vilio kwa kitendo alichokifanya mwanaume huyo cha unyama wa kupitiliza.
Maumivu ya kufa! Akiwa ananyonyesha kichanga wake, dakika chache mwanamama Neema Iwena hakujua kama angenusurika kufa baada ya kukatwa shingoni, kichwani kisha kufyekwa mguu wa kulia na mumuwe, Victor Nzali, kisa kikidaiwa ni wivu wa kimapenzi.
Mmoja wa majirani wa wanandoa hao aliyeshuhudia tukio hilo ambaye aliomba hifadhi ya jina gazetini alisema kwamba, tukio hilo baya maishani lilitokea hivi karibuni ambapo mwanaume huyo alikuwa akimshutumu mkewe kwamba ana mchepuko nje ya ndoa.Neema Iwena akiwa na mwanaye mchanga katika Hospitali ya Rufaa ya St. Francis, Ifakara.
Alisema kwamba, siku ya tukio, Victor ambaye alikuwa akituhumiwa kumtesa mkewe alifika nyumbani na kuanza kuzozana na mkewe kabla ya kuchukua uamuzi mgumu wa kumkata mapanga.
“Unajua alishazoea kumpiga mkewe lakini hii ya kipindi hiki ilikuwa hatari sana.
“Yaani huyu mama ameponea chupuchupu. Mumewe alianza kwa kumkata shingo kwa nyuma. Aliposhindwa na kumwachia jeraha kubwa na damu nyingi ikimwagika ndipo akahamia kichwa, napo akamwachia jeraha.Jeraha la panga la utosi alilopigwa Neema Iwena.
“Yote hiyo akaona haitoshi, akaamua kumfyeka mguu kwa kutumia panga kali.
“Unajua alikatia kwenye goti sehemu penye ‘jointi’ na kuuondoa kabisa.
“Yaani kisa ni wivu wa kimapenzi tu na isitoshe wana mtoto mchanga wa miezi miwili, jamani inasikitisha kwa kweli. Ukimuona lazima utalia kwa jinsi inavyouma,” alisema jirani huyo huku akiangua kilio.Akizungumza kwa uchungu usioelezeka, akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya St. Francis, Ifakara, Neema mwenye umri kati ya miaka 20 hadi 25 alisema kwamba mumewe ndiye aliyemsababishia ulemavu wa mguu kutokana na wivu wa kimapenzi.Waziri wa Wanawake Jinsia na Watoto, Sophia Simba akizungumza jambo. Neema alisema anashukuru kwa sababu anaendelea vizuri tofauti na alipofikishwa hospitalini hapo hali yake ikiwa mbaya kupita maelezo.“
Jamani naombeni Watanzania wanisaidie kwa hali na mali, nimepata ulemavu wa maisha na sina msaada wowote na maisha yangu ni magumu, isitoshe nina mtoto mdogo na Victor baada ya kunifanyia unyama huu, alitoweka, sijui alipo na hajakamatwa pamoja na kwamba tumeripoti polisi,” alisema Neema ambaye hajui kipande cha mguu kilichokatwa kipo wapi.
Alimuomba Waziri wa Wanawake Jinsia na Watoto, Sophia Simba, wanaharakati, wasamaria wema na mamlaka zinazohusika kumsaidia kwani alizaliwa na viungo vyote lakini sasa ni mlemavu kwa sababu asiyoijua kwani hajawahi kuwa na mwanaume mwingine zaidi ya Victor ambaye alimkabidhi moyo wake.
Kwa mujibu wa daktari wa hospitali hiyo aliyolazwa, Neema alifikishwa hospitalini hapo na ndugu zake hali yake ikiwa mbaya mno lakini kwa sasa Mungu mkubwa kwani anaendelea vizuri.
Kwa yeyote anayeguswa kumsaidia Nemaa anaweza kuwasiliana au kutuma chochote kupitia namba ya baba yake: 0689 837 162. Hujafa hujaumbika na kutoa ni moyo si utajiri
No comments:
Post a Comment