WATU wawili, Dilu Tungu (80) na mwanawe Bunya Mihangwa (45) wameuawa kikatili kwa kuchinjwa na watu wasiofahamika baada ya kuvamia nyumba hiyo katika kijiji cha Ihugi kata ya Lyamidati wilaya ya Shinyanga kwa kile kilichoelezwa kuwa ni imani za kishirikina.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 14 mwaka huu saa mbili usiku katika kijiji cha Ihugi, kata ya Lyamidati tarafa ya Nindo wilaya ya Shinyanga.
Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo alisema siku hiyo, Dilu na mtoto wake Mihangwa, wote wakazi wa Ihugi wakiwa nyumbani kwao wakijiandaa kwa chakula cha usiku na wanafamilia wenzao walivamiwa na watu watatu wasiofahamika wakiwa na mapanga.
“Baada ya kuwavamia walianza kuwakata kwa panga sehemu mbalimbali za miili yao kisha kuwachinja shingo hadi wakapoteza maisha,” alisema Kamanda Kamugisha.
Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina kutokana na kile kilichodaiwa kuwa mwanamume aitwaye Bwanya Mlyashimba (40), mkazi wa Ihugi alikuwa akiwatuhumu Dilu na mwanawe Mihangwa kwamba walimroga yeye mwenyewe na kusababisha akose nguvu za kiume.
Alisema mbali na Mlyashimba kuwatuhumu kumroga, pia alikuwa anawatuhumu kumroga mama yake aitwaye Hollo Mahangwa aliyefariki dunia mwaka 2013.
Akasema Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi huku likiendelea kuwasaka wahusika wengine wa mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment