Mitaani kuna miwani ya aina nyingi inayouzwa kienyeji na watu wengi wamekuwa wakiinunua na kuivaa kama urembo au kupunguza makali ya miale ya jua. Kuna wengine huvaa pia ili watu wasiwatambue.
Kiafya, miwani hii ambayo ina kioo cha kawaida na inauzwa mitaani, haina athari kubwa kwa mtumiaji. Mingine husaidia kupunguza miale ya jua.
Miwani ya hatari ni ile yenye kioo cha lenzi ambayo ukiivaa inabadili uono. Ukiivaa inaweza ikakifanya kitu unachoangalia kikawa karibu zaidi au kukiweka mbali zaidi kuliko uhalisia.
Nimeamua kuzungumzia suala hilo kwa sababu kuna watu wanaouza kienyeji miwani ya kusaidia wenye matatizo ya kuona kwa kuwaambia wafanye majaribio ya kuvaa hadi watakapopata miwani inayowasaidia kuona na kusoma.
Hivyo ni hatari kwa sababu unaweza kuathiri macho na kusababisha tatizo lake kuwa kubwa zaidi.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa kila tatizo la macho lina hatua zake hivyo halina budi kufanyiwa marekebisho kwa miwani inayolingana na hali halisi ya kiwango cha kasoro ya uono kwa wakati huo.
Kaam una tatizo la kuona, kusoma au kuumia macho unapotazama mwanga, jaribu kwenda kwa mtaalamu wa macho ili akusaidie kuliko kuhatarisha macho yako kwa kubahatisha miwani mitaani.
No comments:
Post a Comment