LIGI ya soka ya Daraja la Kwanza Tanzania Bara inaanza leo katika viwanja tisa tofauti katika miji kadhaa nchini, ikishirikisha timu 23 zinazowania kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Ligi hiyo itashirikisha timu 23 zilizogawanywa katika makundi mawili; Kundi A likiwa na Tessema FC (Dar), African Lyon (Dar), Majimaji (Songea), Polisi Dar es Salaam, Ashanti United (Dar), Friends Rangers (Dar), Mlale JKT (Songea), Kurugenzi Mafinga (Njombe), African Sports (Tanga), Kimondo FC (Mbeya) na Villa Squad (Dar).
Kundi B lina timu za Panone FC (Moshi), Mwadui (Shinyanga), Geita Gold SC (Geita), Kanembwa JKT (Kigoma), Green Warriors (Dar), Rhino Rangers (Tabora), Toto African (Mwanza), Polisi Dodoma (Dodoma), Burkina Faso (Morogoro), JKT Oljoro (Arusha), Polisi Mara (Mara) na Polisi Tabora (Tabora).
Timu nne zitapanda kucheza Ligi Kuu msimu ujao wa 2015/16 zikijumuika na timu 12 zitakazobaki msimu huu kufanya jumla ya timu 16 baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongeza timu katika ligi hiyo kubwa.
Tunazitakia kila la heri timu zote 23 zinazoshiriki ligi hiyo kwa kuwamo katika Ligi ya Daraja la Kwanza, lakini zaidi tukiamini zimejiandaa vya kutosha katika kuhakikisha zinafanya vizuri na zile nne za kwanza zinacheza Ligi Kuu.
Lakini zaidi tunaamini zitaheshimu sheria 17 za soka duniani ambazo zitatawala muda wote wa michuano hiyo na hivyo kuwapa burudani mashabiki wa soka watakaojitokeza kwenye viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo itakuwa ikichezwa na hivyo mashabiki kujionea burudani safi, na siyo vurugu.
Soka ni mchezo wa kiungwana na wenye kusisitiza suala la amani, upendo na mshikamano, hivyo hakuna sababu ya kushuhudia mechi zilizogubikwa na vurugu.
Ni lazima timu zijiepushe na hali hiyo, lakini pia kwa mashabiki wao, lazima waheshimu taratibu za uendeshaji wa mpira wa miguu duniani.
Si hao tu, waamuzi pia wazingatie sheria 17 za soka ili timu inayostahili kushinda, ndiyo ipate ushindi badala ya kuzibeba timu ambazo hazina uwezo kwa sababu ama ya kuhongwa, kujuana na viongozi wa timu hiyo au kusukumwa kwa namna yoyote ile na kitu kingine, badala ya sheria zinazotawala mpira wa miguu.
Ni vyema waamuzi wakaepuka hilo ili timu zinazopanda Ligi Kuu ziwe timu zilizojimudu zenyewe kiuwezo uwanjani.
Kwa TFF, wanapaswa kusimamia sheria, kanuni na taratibu za mchezo wa soka na zile zinazoongoza Ligi Daraja la Kwanza msimu huu ili kuepuka mambo yanayoweza kuharibu ligi hiyo.
Kwa mfano, msimu uliopita, kuna rufaa ilicheleweshwa kutolewa maamuzi na hivyo kuzua maneno yaliyoashiria kulikuwa na hila za kuibeba timu mojawapo.
Hii ni dosari kwani ucheleweshaji wa haki ni sawa na kumnyima mtu haki, hivyo maamuzi yoyote yanapaswa kutolewa mapema ili kuondoa hisia hizo za kubeba timu mojawapo. Lakini pia TFF iwe wakali kwa waamuzi wake ili kuhakikisha wanatenda haki na kuifanya ligi hii iendeshwe kwa misingi ya haki. Kila la heri.
No comments:
Post a Comment