MTUHUMIWA wa matukio ya kigaidi na umwagiaji watu tindikali katika miji mbalimbali nchini ikiwa pamoja na Arusha, Yahaya Hassan Hela (31) maarufu kama Yahaya Sensei amezikwa usiku wa `manane’ kijijini kwao Chemchem, kata ya Suruke wilayani Kondoa, Dodoma.
Sensei aliuawa na polisi wakati akijaribu kuwatoroka baada ya kupambana nao wakiwa kwenye gari.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, akiwemo shemeji wa marehemu aliyekataa kutajwa jina gazetini, mwili wa Sensei ulizikwa juzi saa 6 usiku kwa kile kilichoelezwa wanandugu walihofia kusumbuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Mtoa habari wetu ambaye ni mkazi wa kata ya Daraja Mbili jijini Arusha, alisema alipigiwa simu na baba mzazi wa Sensei, Mzee Hassan Hela aliyeamuru mwili wa mtoto wake usafirishwe na kufikishwa kijijini kwao haraka.
Alisema mwili wa Sensei aliyeuawa baada ya kupambana na polisi usiku wa kuamkia Jumatatu wakati akisafirishwa kwenda Kondoa ili aoneshe sehemu ya mabomu aliyoyaficha huko, ulichukuliwa hospitali juzi saa 5 asubuhi hadi Daraja Mbili tayari kwa kusafirishwa kuelekea kijijini kwa maziko.
‘’Tulimzika juzi usiku kutokana na mwili kuharibika na isingekuwa busara kuacha hadi siku inayofuata na watu waliohudhuria hawakuwa wengi.
“Ukiondoa sababu hiyo, ndugu waliamuru mwili uzikwe usiku wa saa 6 kwa sababu za kiusalama,” alisema mtoa habari huyo aliyeongeza kuwa, licha ya kuuhifadhi mwili wa Sensei usiku mwingi, lakini taratibu zote za kidini zilifuatwa.
Sensei aliyekuwa mwalimu wa kareti na judo mwenye cheo cha `Mkanda Mweusi’ katika fani hiyo, alikuwa mkazi wa Mianzini, Arusha aliuawa baada ya kutumia taaluma yake hiyo kupigana na Polisi wakiwa garini majira ya saa 5 usiku na aliporuka kutoka kwenye gari aweze kukimbia, polisi walimuwahi kwa risasi na kumsababishia mauti.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani, Liberatus Sabas, Sensei alikamatwa baada ya kukiri kuhusika katika matukio tisa ya ulipuaji wa mabomu na umwagiaji watu tindikali katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.
Shekhe Farid Wakati mtuhumiwa huyo akizikwa huko Kondoa, jijini Dar es Salaam Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kutoa uamuzi wa ombi la kufutiwa mashitaka ya ugaidi yanayomkabili Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho, Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake kwa kuwa jalada halisi la kesi hiyo limepelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa kwa ajili ya kutolewa kwa uamuzi wa ombi hilo lililokuwa limewasilishwa na washitakiwa ambapo Hakimu Riwa alisema hawezi kutoa uamuzi wa ombi hilo kwa sababu jalada halisi la kesi hiyo limeitishwa Mahakama Kuu, akaahirisha kesi hadi Novemba 4 mwaka huu itakapotajwa tena.
Washtakiwa hao waliwasilisha ombi wakiiomba Mahakama ifute kesi hiyo kwa sababu hati ya mashitaka iliyopo mbele ya mahakama hiyo ina mapungufu.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni kiongozi mwingine wa Jumuiya hiyo Shekhe Mselem Mselem ambaye pamoja na Shekhe Ahmed wanatuhumiwa kuwaajiri watu waliotenda vitendo vya kigaidi.
akiwamo Abdallah Said Ali. Katika mashita mengine yanayowakabili pamoja washitakiwa wengine 19, inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2013 na Juni, 2014 katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washitakiwa wote walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, kwa kuingiza watu kushiriki vitendo vya kigaidi.
Aidha, washitakiwa wanadaiwa kuwasaidia watu hao kufanya vitendo vya ugaidi.
HABARI LEO.
No comments:
Post a Comment