Sunday, 28 September 2014

WAHALIFU WANAOTUBU KANISANI KURIPOTIWA POLISI



KANISA Anglikana linakabiliwa na shinikizo la kutakiwa kulegeza masharti ya sheria zake ili wachungaji waweze kuripoti uhalifu wanaousikia kutoka kwa waumini wao wanaoungama. Utaratibu huo umeshaanza kutekelezwa na Kanisa Anglikana Australia ambalo limeruhusu wachungaji kuripoti polisi uhalifu uliobainika wakati wa maungamo ya waumini.



Askofu wa zamani wa kanisa hilo, Dayosisi ya Chelmsford, Jimbo la Canterbury, John Warren Gladwin ni miongoni mwa wanaoshinikiza kulegezwa kwa sheria hiyo ya kanisa ili kuwezesha makosa makubwa kama vile udhalilishaji watoto yanayotokana na waumini walioungama, yaripotiwe polisi.
Akisifu kanisa la Australia kwamba limekuwa mfano mzuri sana, askofu huyo anataka kanisa lihakikishe mabadiliko hayo yanatokea na yanafanya kazi.
Gladwin ambaye mwaka jana aliongoza jopo la kuchunguza tuhuma za udhalilishaji kingono uliodaiwa kufanywa na viongozi wa dini ndani ya Kanisa la Anglikana, sanjari na wajumbe wa mkutano mkuu, anashinikiza mabadiliko hayo.
Askofu huyo wa zamani ambaye ripoti yake kwa Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby ilisababisha kuomba msamaha kwa waathirika wa udhalilishaji, alisisitiza, “ni muhimu jambo lolote la uhalifu, linalohusiana na udhalilishaji watu kutolindwa. Hatua lazima zichukuliwe.”
Kwa miongo kadhaa usiri wa kuungama kimadhehebu unatajwa kuwa ni utakatifu ingawa inaelezwa Kanisa la Anglikana linaweza kulegeza sheria kuruhusu viongozi wa dini kubainisha matukio makubwa ya kiuhalifu.
Julai mwaka huu, katika mkutano mkuu, Kanisa Anglikana Australia lilipiga kura kuruhusu mapadri kwenda polisi kama mtu aliyeungama atakataa kwenda kujisalimisha, likisema usalama wa waathirika wa matukio hayo ya uhalifu ni jambo kubwa.
Uhalifu huo ni pamoja na udhalilishaji watoto, ngono kwa watoto au makosa mengine kama hayo ambayo yatasababisha mkosaji kufungwa jela miaka mitano au zaidi. Dayosisi ya Australia inatarajiwa kuanza kutekeleza mabadiliko hayo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu .
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Canterbury, Welby mwaka jana pia aliomba Waanglikana zaidi kupitisha utaratibu huo licha ya kwamba, zaidi ya miaka 400 mapadre wamekuwa wakizuiwa na Sheria ya Kanisa kutoa ‘siri na dhambi’ ikiwemo uhalifu, zilizotolewa na wanaoungama.
Inaelezwa hoja ya kutaka sheria za kanisa kufanyiwa marekebisho ili wachungaji wasiwe na mamlaka tena ya kufanya maungamo ya udhalilishaji kuwa siri, inatarajiwa kufikishwa kwenye Mkutano Mkuu wa kanisa Novemba mwaka huu.
Mjumbe wa mkutano huo, Mchungaji Simon Cawdell, amekiri kupeleka hoja akitaka Sheria za Kanisa zifanyiwe marekebisho ili mapadre wasiwe na mamlaka tena ya kuficha maungamo ya udhalilishaji.
Msemaji wa Kanisa Anglikana anakiri kwamba miongozo ya wachungaji inafikiriwa kujadiliwa katika mkutano huo na zaidi uamuzi wa Australia, utakuwa miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa.
Wachambuzi wa masuala ya kanisa hilo wanasema mabadiliko yoyote yatapingwa vikali na wanaozingatia taratibu za jadi za kanisa ambao wanafikiri kiongozi wa dini anapaswa kuheshimu imani waliyonayo waumini kwa viongozi wa dini.
Vile vile marekebisho hayo yanatajwa kwamba yatasababisha mvutano na Kanisa Katoliki ambalo linaamini maungamo ya muumini yanapaswa kulindwa na kubakia kama utaratibu ulivyo.
Sakramenti ya kitubio ambayo muumini hukiri kwa siri dhambi zake kwa padre, mara nyingi huhusishwa na Kanisa Katoliki.
Hata hivyo taarifa zilizopo ni kwamba, robo ya mapadre wa Anglikana kwa kawaida husikiliza maungamo kwa kukaa ana kwa ana katika chumba binafsi kuliko kibanda ndani ya kanisa.
Wapo viongozi wa ngazi za juu za kanisa Anglikana wanaoweka bayana kwamba kufuata utaratibu wa Australia ni kuharibu ukuhani. Mmoja wa viongozi wa Sinodi alikaririwa akisema,
“kama tutafuata njia ya Australia tutaharibu ukuhani.Unatakiwa kwenda kwa padre na kumwaambia kila kitu. Huu ni utaratibu wa Kanisa Katoliki na tumeufuata wakati wote.Kama tutafanya kitu tofauti sasa tutamkwaza kila mtu.”
Askofu wa Kanisa Katoliki, Arundel na Brighton, Kieran Conry alisema mabadiliko ya Kanisa Anglikana yanaweza kuleta shinikizo kwa kanisa lao pia kuchukua hatua hizo ingawa alisisitiza, “Hautuwezi kamwe kulegeza kabisa mahitaji ya usiri.”

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!