Wednesday, 24 September 2014
VIFO BARABARANI VYAISHTUA SERIKALI
SERIKALI imesema inahitajika mikakati kukabili ajali za barabarani kwani kwa sasa vifo vitokanavyo na ajali vimekuwa janga linalozidi vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Ukimwi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima alisema serikali sasa inawekeza zaidi kwenye mapambano dhidi ya vifo hivyo.
"Kutakuwa na ukaguzi wa lazima kwa kila gari, kuwepo kwa kamera za kutosha na vipima ulevi ambavyo vimeshawasili ili kutimiza kampeni ya usalama barabarani," alisema.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya hundi ya Sh milioni 40 kutoka kwa Kampuni ya Mafuta ya Puma kuwezesha Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani.
Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Arusha.
Alisema matukio ya ajali yanayotokea kwa sasa yanaligharimu Taifa kutokana na vifo vyake kuzidi vya janga la Ukimwi hivyo Serikali kuwekeza zaidi katika mapambano.
"Puma ni mfano mzuri kwa makampuni yenye kuhitaji maendeleo ya nchi, kwani vita dhidi ya ajali za barabarani ni vita inayotakiwa kuungwa mkono na wadau wote wa maendeleo kutokana na vifo vyake kuwa vingi na taifa kupoteza nguvu kazi," alisema.
Aliongeza kuwa uwepo wa ajali hizo haumaanishi Serikali na jeshi la polisi limelala, hivyo mikakati iliyopo itahakikisha utoaji wa leseni kwa madereva wa mabasi ya abiria mkoani unazingatia mafunzo ya kutosha.
Meneja wa Puma, Phillipe Corsaletti alisema kampuni hiyo imeungana na serikali kupambana na ajali za barabarani. Alisema wanatarajia kuingia mkataba wa miaka mitano wa kampeni ya kupunguza ajali nchini
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment