Monday, 15 September 2014

MWAKYEMBE AUNDA TUME YA AJALI



WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameunda Kamati Maalumu iliyopewa kazi ya kuchunguza mambo mbalimbali ambayo yatasaidia kupunguza ajali za barabarani.



Akizungumza baada ya mkutano wa wadau wa sekta ya usafirishaji jana, Dk Mwakyembe alisema kamati hiyo itafanya kazi usiku na mchana kwa wiki mbili na Oktoba 5 yeye mawaziri wenzake, Gaudentia Kabaka wa Kazi na Ajira na Mathias Chikawe wa Mambo ya Ndani watakutana ili watoe maamuzi mbalimbali yatakayosaidia kupunguza tatizo la ajali.
Kamati hiyo inaundwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi ambaye pia atakuwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna wa Mapato Nchini (TRA), Kamishna Mkuu wa Wakala wa Bima, Mwakilishi wa Wamiliki wa Mabasi (Taboa).
Mtendaji wa Wakala Barabarani Nchini (TANROADS) ni miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA, Mtendaji Mkuu wa VETA, Mtendaji Kitengo cha Matokeo Makubwa Sasa na Mwakilishi wa Wamiliki wa Malori (TATOA).
Alisema hadidu za rejea za tume hiyo ni kubaini changamoto katika utayarishaji wa ratiba za mabasi zinazotolewa na Sumatra ambazo kwa sasa baadhi yake zinaghushiwa na namna bora ya kutumia Tehama katika utayarishaji na udhibiti wa ratiba.
Tume hiyo pia itathmini uwezekano wa muda halali wa mabasi kusafiri, kutathmini mwendo wa ukomo wa mabasi, kutathmini upatikanaji wa leseni ya madereva daraja C ambazo ilidaiwa kwenye kikao hicho kuwa zinauzwa ovyo Kariakoo.
Kutathmini huduma za magari yenye uwezo mdogo wa kubeba abiria ambayo kwa sasa yanafanya safari ndefu kuliko uwezo wake. Alitoa mfano magari kama Noah linafanya safari kutoka Tunduma hadi Sumbawanga zaidi ya kilometa 300.
Pia tume hiyo itatathmini ajira za madereva na muda wa kazi ambao wanatakiwa kufanya kazi. Kazi nyingine watatathmini ukaguzi wa lazima wa mabasi na malori, kutathmini mfumo wa bima kwa mabasi ya abiria, tathmini alama za barabarani, utaratibu wa kupima mabasi kwenye mizani na vituo vya ukaguzi.
Kutathmini matumizi ya tehama katika ukusanyaji wa faini kwa makosa mbalimbali ya barabarani, ushirikiano wenye tija kati ya Sumatra, Polisi na Taboa.
Dk Mwakyembe alisema Sumatra itatoa sekretarieti na kazi wataifanya kwa siku 14 kuanzia Ijumaa ijayo na kwamba ifikapo Oktoba Mosi, ripoti itakuwa mezani kwa Dk Mwakyembe.
Alitoa maamuzi mengine ambayo alisema hayahitaji kamati na kwa kuanzia, Sumatra na trafiki wahakikishe dereva wa gari lolote haendeshi gari huku anazungumza na simu.
Akaagiza kwamba dereva akionekana anaongea kwa simu akamatwe na abiria watoe taarifa. Akasisitiza kwamba hiyo ni sheria ya siku nyingi, lakini haitekelezwi.
“IGP hakikisheni hilo linazingatiwa kwa madereva wote sio wa mabasi tu, polisi kuweni wakali kulisimamia hilo, madereva wote wa malori, mabasi, magari madogo…hata kama nyinyi waandishi pia mnaongea na simu huku mnaendesha, tutawakamata,” alisema Mwekyembe.
Kwa upande wake, IGP Mangu akijibu tuhuma za ukosefu wa uadilifu wa trafiki, alisema Polisi haiwalei polisi ambao sio waadilifu na akaomba ushirikiano kutoka kwa waathirika wa mwenendo mbaya wa askari hao ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa.
Mkuu huyo wa Polisi aliwashutumu wamiliki wa mabasi kuwa, wapo wamiliki wa mabasi wamewaweka askari kwenye orodha ya malipo (payroll) ili wasikamate mabasi yao. Alitaja sababu kubwa ya ajali mwendo kasi na kuyapita magari mengine bila ya uangalifu.

1 comment:

Anonymous said...




1
Reply

Well done Mr Mwakyembe,keep up the good work.

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!