Katika hali isiyo ya kawaida, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanadaiwa kuwafanyia ukatili mkubwa vijana 11, wakazi wa eneo la Keko Magulumbasi B, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kwa kuwapiga na kuwalazimisha wanywe maji machafu yenye kinyesi.
Tukio hilo ambalo limefananishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, linadaiwa kutokea Septemba 12 mwaka huu, saa 11 jioni, katika eneo la Keko Magulumbasi B.
Inadaiwa kuwa, wanajeshi hao ambao walikuwa saba wakiwa na sare za jeshi hilo, walifika Keko Magulumbasi B wakiwa na kijana mmoja mwenye asili ya Kiarabu na kuwavamia vijana waliokuwa wakila chakula kwenye kibanda cha chipsi.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa, wanajeshi hao waliwakamata vijana hao na kudai wanahusika kupora simu ya kijana mwenye asili ya Kiarabu aina ya Tecno yenye thamani ya sh. 25,000.
Pamoja na vijana hao kukataa kuhusika na tukio hilo, waliwekwa chini ya ulinzi, kufungwa mikono kwa kamba, kulazwa kifudifudi na kuanza kupigwa mikanda ya jeshi.
Mashuhuda hao waliongeza kuwa, vijana hao walichukuliwa hadi kwenye bwawa la maji machafu yaliyochanganyika na kinyesi cha binadamu wakazamishwa vichwa vyao ndani ya bwawa hilo la kulazimishwa kunywa maji hayo.
Waliongeza kuwa, vijana hao wakiwa wamelowana kwa maji machafu walichukuliwa na wanajeshi hao hadi Kituo Kidogo cha Polisi Keko na kuswekwa rumande na mmoja wao aliachiwa baada ya dakika 10.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walilazimika kuvamia kituo hicho na kufanya vurugu wakiwarushia mawe askari wa kituo hicho kwa lengo la kuwatoa vijana hao kwa nguvu wakidai wameonewa.
Hata hivyo, wananchi hao walitawanywa kwa risasi za moto zilizopigwa hewani na askari wa Kituo Kikuu cha Polisi Chang'ombe walioitwa kuongeza nguvu kituoni hapo.
Bw. Omary Abdu (30) ambaye ni mkazi wa eneo hilo ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio, alidai kutofurahishwa na kitendo kilichofanywa na wanajeshi hata kama vijana hao wameiba kwani walipaswa kufikishwa katika mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.
"Walichokifanya wale wanajeshi ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na haki za binadamu...naamini wanafahamika, itakuwa vizuri kama watachukuliwa hatua za kisheria," alisema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliwashutumu wakazi wenzake kwa kitendo cha kuvamia Kituo cha Polisi na kufanya fujo kwa kuwarushia mawe polisi.
Katika hatua nyingine, mkazi huyo alimtuhumu Mwenyekiti wa Mtaa wa Magulumbasi B, Bw. Mohamed Fundi ambaye alidai kupitia kikao chake na wananchi Agosti 29 mwaka huu, alihamasisha wagome kukamatwa na polisi.
Alidai kauli kama hiyo inaweza kuleta vurugu na uvunjifu wa amani hivyo zinatakiwa kukemewa na kila mkazi wa eneo hilo.
Mwandishi alimtafuta Bw. Fundi ambaye alikiri kufanya kikao na wananchi kwa tarehe hiyo ambacho kilikuwa na lengo la kuhamasisha maendeleo na kuwafahamisha wananchi haki zao si kuhamasisha vurugu au kuzuia wasikamatwe na polisi kama inavyoelezwa.
Alisema miongoni mwa haki hizo ni namna polisi anavyotakiwa kumkamata raia na asikamatwe usiku bila kuwepo kwa kiongozi wa eneo lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kihenya Kihenya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akidai taarifa alizonazo ni kwamba, vijana waliokamatwa wanajihusisha na wizi wa mifukoni.
Alisema wakiwa Kituo Kidogo cha Polisi Keko, wananchi walikivamia na kufanya vurugu hadi walipotawanywa na askari kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Chang'ombe kwa kupiga risasi hewani.
"Taarifa zinazosema vijana hao waliteswa na kunyweshwa maji machafu na wanajeshi bado sijazipata ila hawa vijana wanashikiliwa Kituo cha Polisi Chang'ombe wakisubiri kufikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika," alisema.
Inaelezwa kuwa, wiki moja iliyopita kijana huyo mwenye asili ya Kiarabu mkazi wa Keko Toroli, alivamiwa na vijana eneo la Keko Magulumbasi B, ambao walimpora simu ya mkononi tukio ambalo liliripotiwa kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Keko.
Chanzo: Majira
1 comment:
aziz bilal18:46
1
Reply
Hilo linachangiwa sana na tatizo la kutokuwa na ajira,hao vijana inavyoonekana ni vibaka tena wa kujulikana na kitendo cha askari wa jeshi kuwashughulikia si sahihi.
Post a Comment