Friday, 8 August 2014

VIJANA WENGI HAWANA UELEWA WA VVU



NUSU ya vijana wenye miaka kati ya 15-24 katika maeneo mengi hapa nchini wanakabiliwa na changamoto ya uelewa duni kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi na afya ya uzazi, hali inayokwamisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo miongoni mwa jamii.


Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk. Leticia Warioba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya mradi wa kipindi cha redio kijulikanacho kama ‘Shuga’.
Dk. Warioba, alisema ukimwi ni miongoni mwa changamoto kubwa katika sekta ya afya na maendeleo, huku akibainisha kuwa kundi la vijana licha ya ukubwa wake bado halijapewa msukumo zaidi, hasa katika eneo la matumizi ya kinga.
Alisema kuwa mradi huo umekuja wakati muafaka, ambako malengo yake yakizingatiwa na kutekelezwa kama ilivyopangwa, utasaidia kufikia malengo ya serikali ya kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi hadi kufikia sifuri, ikiwa imewalenga zaidi vijana wenye miaka 15 na kuendelea.
“Lengo kuu la kampeni ni kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU, miongoni mwa vijana wa umri wa kubalehe kupitia vyombo vya habari na kuwafikia kwa ujumbe mahususi kuhusu upimaji wa hiari na ushauri nasaha na ngono salama,” alisema Dk. Warioba.
Aliongeza kuwa, redio za jamii ni kiungo muhimu katika kuelimisha jamii na kwamba, kama zitatumika vizuri kusambaza elimu ya ukimwi kupitia vipindi vyake, zitasaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali kupitia Tacaids.
Kwa upande wake, Victor Chakudika ambaye ni Meneja wa Nuru Fm ya mkoani hapa watakaorusha kipindi hicho, alivitaka vyombo vya habari nchini kuongeza juhudi katika kuandika na kutangaza habari za kuelimisha jamii kuhusu maambukizi ya VVU.
Mradi wa kipindi cha ‘Shuga’, unaendeshwa na Unesco kwa kushirikiana na UNICEF na una lengo la kuwajengea uwezo vijana kuhusu masuala ya VVU na afya ya uzazi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!