Tuesday, 5 August 2014

UGONJWA WA EBOLA INAVYOTIKISA AFRIKA




Conakry. Wakati wakuu wa mataifa ya Guinea, Sierra Leone na Liberia wanakutana kwenye mji mkuu wa Guinea, Conakry kwa ajili ya kungalia jinsi gani ya kupambana na ugonjwa wa ebola, Shirika la Afya Dunia (WHO), limetangaza kutoa Dola za Kimarekani 100 milioni ili kukabiliana na janga hili ambalo hadi sasa limegharimu maisha ya Waafrika zaidi ya 730.
Pia hali bado ni tete kwani ugonjwa huo unaendelea kuathiri watu wengi zaidi.WHO na viongozi hao wa mataifa athirika, walikutana Ijumaa kuangalia jinsi gani ya kutumia pesa hizo kwa mapambano ya ebola.

Katika mkutano huo wa viongozi wa Afrika imeelezwa kuwa kazi kubwa ni kuangalia jinsi gani ya kupambana na ugonjwa huo kwa ndani na kuweka mkazo maeneo ya mipakani ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Kufanyika kwa mkutano huo ni baada ya mamlaka za afya za Marekani, Ujerumani na Ufaransa kutoa tahadhari kwa watu kusafiri katika mataifa hayo matatu yaliyoathiriwa na ugonjwa huo.
“Ni kama kupambana na moto wa nyika. Kama ikimalizika hatua moja ya mapambano, kwengine mambo yanaibuka upya,” alisema Tom Frieden, mkuu wa Kitengo cha Afya wa Marekani.
Wakati hayo yakifanyika, mataifa mbalimbali ya Afrika yameanza kuchukua tahadhari kuhusiana na ugonjwa huo.
Hapa nchini, Serikali iliwaita maofisa mbalimbali wa afya kuzungumzia tahadhari za kuibuka kwa ugonjwa wa ebola.
Hata hivyo, kikubwa kilichopangwa ni kwamba, wahusika hao wa sekta ya afya wamepanga kuweka mkakati katika maeneo ya viwanja vya ndege vya Zanzibar, Dar es Salaam na Kilimanjaro.
Afrika Kusini imetoa msimamo wake kwamba haitahudumia mgeni yeyote atakayewasili nchini humo akiwa na viashiria vya ugonjwa huo, kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza (NICD).
Nigeria imetangaza kuweka karantini baada ya kuonekana kwa watu wawili wenye dalili za ebola kwenye mji wa Lagos.
Nchini Rwanda, Waziri wa Afya, Dk Binagwaho na Waziri wa Uchukuzi, James Musoni juzi walitembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali kukagua utayari wa watumishi wa afya uwanjani hapo na maandalizi endapo itatokea mtu mwenye viashiria vya ebola.
Uwanjani hapo, tayari kumewekwa gari la wagonjwa, pamoja na manesi waliopata mafunzo maalumu katika hospitali za kijeshi Rwanda pamoja na kuwapo na chumba maalumu chenye zana zote za huduma za kwanza kwa mwathirika wa ebola.
Maeneo ya viwanja vya ndege, maofisa uhamiaji wamekwishapewa maelekezo ya jinsi ya kumsaidia mgonjwa wa ebola hasa kwa wale wanaotoka Afrika Magharibi. Idara ya Uhamiaji imeweka utaratibu mpya kwa wanaoingia nchini humo kujaza fomu maalumu kwa wasafiri wanaoingia Rwanda.
“Wasafiri wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao za ugonjwa wanapoingia ama kutoka, kuonyesha kuwa ulihudhuria maziko ya ndugu wa karibu ndani ya wiki ama mwezi mmoja uliopita au kama ulikuwa na ndugu aliyekuwa anaumwa magonjwa ya milipuko. Anuani ya mwenyeji wa mgeni Rwanda ambayo yanatakiwa maelezo ya kina.
Baada ya ukaguzi wa viwanja vya ndege, Binagwaho alizungumza na wamiliki wa hoteli nchini Rwanda kwenye Hoteli ya Sports View kuhusu hali hiyo.
Wamiliki hao walitakiwa kutokuwa na wasiwasi na kwamba watoe taarifa kwa mamlaka za afya pindi wanapomwona mtu mwenye dalili za ebola (homa kali, kulegea, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa, kutapika, kuhara na kutoa damu sehemu mbalimbali za mwili).
Huko Uganda, Waziri wa Afya, Dk Ruhakana Rugunda, tayari ameshaunganisha nguvu na maofisa wa Shirika la Afya (WHO) kwa Afrika kuhusu ugonjwa huo.
Nchini Kenya, Waziri wa Afya aliwahakikishia Wakenya kutokuwa na wasiwasi kwani wahusika wamejipanga kukabiliana na kuzuka kwa ebola. Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Nicholas Muraguri anasema Mamlaka za Afya zimewekwa katika tahadhari kubwa endapo itatokea ugonjwa huo.
Wafanyakazi wa Kenya Airways, wamepewa mafunzo jinsi ya kumsaidia mgonjwa wa ebola hasa kwa ndege zinazokwenda Sierra Leone, jinsi gani ya kujikinga na virusi wa ugonjwa huo.
Wahudumu hao wa Kenya Airways wamepewa vifaa vya tahadhari vya Universal Precaution Kits (UPK) kujikinga na maambukizi dhidi ya mtu anayeugua ebola.
Ivory Coast imekuwa katika mkakati mkali kukabiliana na ugonjwa huo. Wadau wa afya nchini humo, wamesema wamekuwa katika uangalizi wa karibu hasa maeneo ya viwanja vya ndege.
Kuna wasiwasi kuwa ugonjwa huo unaweza kuenea katika Afrika na kwingineko kutokana na usafiri wa anga kutoka na kuingia Afrika kwa mabara ya Ulaya na Asia.
Chama cha Madaktari Wasio na Mipaka kimeonya hakuna jitihada za makusudi katika kukabiliana na ugonjwa huo katika ngazi za dunia.
Mataifa ya Ethiopia na DR Congo, yametangaza kuimarisha ukaguzi kwa abiria watakaokuwa na viashiria vya ugonjwa katika maeneo mbalimbali hasa ya viwanja vya ndege.

Tayari mashirika ya ndege ya Pan-African Arik na ASKY yamesitisha safari za ndege kwenda na kutoka Liberia na Sierra Leone, wakati mataifa ya Asia-Pacific ya Hong Kong na Australia zimeimarisha ukaguzi pamoja na kuweka hadhari ya ugonjwa huo.
Monrovia waandamana
Katika hali ya kustaajabisha wananchi katika Jiji la Monrovia, nchini Liberia wameandamana wakipinga maiti za wagonjwa wa ebola kuzikwa katika maeneo hayo.
Wananchi hao wanaitaka Serikali yao kutafuta maeneo ya kuwazika watu wanaokufa na ugonjwa huo mbali na makwao kwa kuwa wanahofu ugonjwa huo utazidi kuenea.
Wanajeshi walilazimika kuwatawanya waandamaji katika jiji hilo wakidai kuwa mkusanyiko kama huo ni chanzo kingine cha kuenea kwa ugonjwa huo.
Watoa misaada wajiondoa
Wakati hali ikiwa tete, watoa misaada (Peace Corps) wapatao 340 walitangaza kuondoka nchini Liberia kwa madai kuwa hali imekuwa nje ya uwezo wao.
Watumishi wawili wa umoja huo waliambukizwa ebola wiki iliyopita na kulazimika kusafirishwa mpaka Marekani kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mmarekani, Patrick Sawyer aliyekuwa akifanya kazi nchini Liberia alifariki Julai 25 mwaka huu akiwa hospitalini nchini Nigeria alipokuwa akitibiwa ugonjwa wa ebola.
Wiki iliyopita, Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf alitangaza kuwa shule zote zitafungwa kwa muda usiojulikana pia Ijumaa kuwa siku ya mapumziko maalumu kwa ajili ya kufanya usafi.
“Nimeiagiza Wizara ya Elimu kuzifunga shule zote mpaka pale hali itakapokuwa shwari, pia siku ya Ijumaa haitakuwa ya kazi badala yake jamii iitumie katika kufanya usafi.
Imeandaliwa na Ibrahim Bakari kwa msaada wa mashirika ya habari

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!