Wednesday, 20 August 2014

TUSISUBIRI EBOLA HADI IINGIE NCHINI!

EBOLA ni miongoni mwa magonjwa hatari duniani, ambao unasambaa kwa kasi na kuzusha hofu hivi sasa kwenye mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Ugonjwa huo, ambao unasambaa kwa kasi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa njia tofauti, ikiwemo kugusana mtu aliyepatwa na ugonjwa huo na kugusa mizoga ya wanyama waliopatwa na ugonjwa huo, ambako hivi sasa umezidi kuwa tishio katika nchi za Afrika.


Kusambaa kwa ugonjwa huo, kumesababisha hofu kubwa duniani baada ya nchi za Afrika Magharibi kuonekana kushindwa kuudhibiti huku zikichukua hatua mbalimbali muhimu ikiwemo kusitisha safari za ndege ndani na nje ya nchi zao.
Mfano mzuri ni Shirika la Ndege la Emirates, ambalo limetangaza kusimamisha kwa muda safari za kwenda Guinea tangu Agosti 2 mwaka huu kwa sababu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi.
Katika tovuti yake, Emirates ilisema haiwezi kuwaweka hatarini abiria na wafanyakazi wake.
Barani Afrika, homa ya Ebola ilianza Guinea na kutapakaa nchi jirani za Sierra Leone na Liberia. Mashirika mawili ya ndege ya Afrika ya Arik Air la Nigeria na ASKY Togo yamekwisha kutangaza kuvunja safari za kwenda nchi zilizoathirika.
Wakati dunia ikizidi kutafakari juu ya homa hiyo katika nchi za Afrika Magharibi, tayari ugonjwa huo umebisha hodi ukanda wa Afrika Mashariki katika nchi jirani ya Rwanda baada ya kugundulika kwa raia mmoja wa Ujerumani akitokea Liberia.
Baada ya kupatikana kwa taarifa hiyo, sisi Tanzania Daima tunatahadharisha kuwa ukiona mwenzako ananyolewa, wewe tia maji. Ina maana kama ugonjwa umeingia kwa jirani zetu basi tusisubiri na sisi ufike ndipo tuanze kuchukua hatua.
Kimsingi, hadi sasa hakuna juhudi na hatua za makusudi na za wazi hapa nchini kujipanga kuzuia na kudhibiti usipenye hapa nchini.
Tanzania Daima, tunaisisitizia serikali kuchukua hatua za haraka kabla mambo hayajatufika shingoni, kwani inaonekana hakuna jitihaada za haraka ambazo zinachukuliwa, kama utolewaji wa elimu kwa wananchi juu ya dalili maambukizi na namna ya kuuepuka.
Licha ya kuitaka serikali kutoa elimu, pia inatakiwa kutekeleza yale wanayozungumza kama walivyoahidi kusambaza vifaa kwenye viwanja vya ndege, mipakani na kutenga maeneo maalum endapo kutatokea mgonjwa wa dharura.
Tanzania Daima, tunaiomba Wizara husika, kupunguza maneno, badala yake izingatie vitendo kuanzia sasa, kwa kuwaelimisha wananchi na kusambaza vifaa kila sehemu yenye urahisi wa kupitisha ugonjwa huo.
Pia, wizara inatakiwa ifafanue kwa kina njia zinazotumiwa kudhibiti ugonjwa huo kwa kushirikiana na wizara nyingine kama Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Tamisemi na nyinginezo, ambako kwa pamoja zitaweka mikakati madhubuti ya kupambana kuhakikisha ugonjwa huo haupati upenyo kuingia nchini.
Tunasisitiza haya, kutokana na uzoefu mbalimbali hapa nchini, ambako magonjwa hatarishi mapya yanapopiga hodi, hali huwa mbaya na hata kuathiri shughuli mbalimbali za wananchi katika ujenzi wa Taifa. Tunasisitiza, tuchukue hatua sasa, tusiisubiri ebola hadi iingie nchini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!