Sunday, 10 August 2014

SERIKALI YAJIPANGA KUKABILI EBOLA

SERIKALI imesema itahakikisha hakuna mwananchi atakayefariki kutokana na kukosa huduma katika vituo vya afya pindi atakapobanika kuwa na ugonjwa wa Ebola labda achelewe kufika katika vituo hivyo.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe wakati alipotembelea bohari ya dawa kujionea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyotolewa na serikali ya Watu wa Marekani kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.

Dk. Kebwe alisema msaada huo umeongeza nguvu katika kupambana na ugonjwa huo ambako awali tayari seriakali ilishajipanga.
Katika mipango hiyo, alisema ni pamoja na kufungwa kwa vifaa vya upimaji wa ugonjwa huo katika viwanja vya ndege, kazi ambayo wanatarajia kuifanya wiki mbili zijazo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Zanzibar, Kilimanjaro na Mbeya ili kuongeza udhibiti.
Alisema kwa Afrika, tahadhari hiyo imekuwa kubwa hasa ukizingatia kwamba hadi sasa wagonjwa wengi wanatoka barani humo ambako inakisiwa Afrika Magharibi imeshapoteza takribani watu 900 kwa ugonjwa huo.
"Dunia imedhamilia kupambana na magonjwa haya na wiki hii tulikuwa kwenye mkutano wa nchi za SADEC ambapo tumebaini vifo vitokanavyo na Ebola ni vingi Afrika Magharibi na kasi ya maambukizi inatokana na tamaduni ambapo kwa nchi za Gunia, Liberia, Sieralion wananchi wamekufa zaidi kutokana na mila za wenza wa marehemu kulala na maiti huku ndugu na jamaa pia wakitaka kushika maiti hizo,”alisema
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi MSD, Cosmas Mwaifwani, alisema katika msaada huo wamepokea jumla ya makasha 320 yenye uwezo wa kutumiwa na wahudumu 16,000.
Mwaifwani alisema vifaa hivyo vina uwezo wa kuwakinga wahudumu wa afya wanapofanya uchunguzi kwa watu wanaodhaniwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo ambako kasha moja lina uwezo wa kutumiwa na wahudumu hamsini.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, tayari hospitali ya Temeke, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Muhimbili, Uwanja wa ndege Mwalimu Nyerere na Mbeya wameshapatiwa vifaa hivyo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!