Tuesday, 12 August 2014

NINI KINAFUATA BAADA YA TANZANIA KUGUNDUA MAFUTA?

Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri wa rasilimali nyingi zikiwamo madini, gesi, mafuta (kuna dalili za kugundulika), misitu, vyanzo vya maji na ardhi yenye rutuba.
Wakati rasilimali zote hizi zikitumika, kwa sasa Tanzania inaendelea na utafiti wa mafuta ambao unaoonyesha matumaini.

Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Tanzania ina jumla ya eneo la kilometa za mraba 534,000 lenye utajiri wa mafuta, likihusisha eneo la pwani lenye ukubwa wa kilometa za mraba 280,000, mabonde ya kina kirefu baharini ukubwa wa kilometa za mraba 140,000, mabonde ya nchi kavu kilometa za mraba 114,000.
Hata hivyo, matumaini hayo nayo yanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za usalama na kidiplomasia.
Katika usalama kuna tishio la uharamia baharini na Ziwa Tanganyika kwa meli za utafutaji, isitoshe mpaka katika ziwa hilo haujakamilika japo unatambulika kisheria
Kwa upande wa utafutaji, Ziwa Nyasa kwa sasa kuna mzozo wa kidiplomasia ambapo Serikali ya Malawi inaonekana kudai kumiliki ziwa lote hivyo kuingia mikataba na kampuni za utafutaji.
Kwa kuwa jiolojia ya miamba haina mipaka kati ya leseni moja na leseni nyingine (ndani ya nchi), pia nchi moja na nchi nyingine (Tanzania na Msumbiji, Tanzania na Kenya; Tanzania na DRC), italazimu taratibu za “mikataba ya Unitization” kufanyika;
Historia ya utafiti wa mafuta
Akizungumzia utafutaji wa mafuta Tanzania, mhandisi mwandamizi wa TPDC, Martin Lumato anasema ulianza mwaka 1952 ambapo Kampuni ya BP na Shell zilianza kazi katika ukanda wote wa pwani. Dalili za mafuta na gesi zilijionyesha kwenye visima walivyochimba Zanzibar na Mafia.
Anasema uchimbaji huo ulifanyika hadi mwaka 1962 ambapo kampuni hizo ziliondoka bila kupata mafuta.
“Kampuni ya Agip nayo ilianza utafutaji wa mafuta mwaka 1962 hadi 1982 ambapo ugunduzi wa gesi ya Songosongo ulifanyika mwaka 1974. Hata hivyo ikasema  gesi hiyo haitoshi na haina faida,” anasema Lumato na kuongeza:
“Lakini,  Shirika letu (TPDC)  wakafanya utafiti zaidi kwa kuchimba zaidi visima 11 vilichimbwa kwa msaada ya Serikali ya India na Benki ya Dunia na kugundua gesi ipo tena ya kutosha. Kama hiyo haitoshi Agip wakagundua tena gesi mwaka 1982 huko Mnazi Bay- Mtwara nayo wakaitelekeza.”
“Kama ulivyo wajibu wake, TPDC na Serikali ikafanya juhudi kubwa kuiendeleza gesi hiyo ikiwa pamoja na kuibadilisha sheria ya utafutaji wa mafuta mnamo mwaka 1980.Mbali na sheria hiyo, Sheria ya Kodi ya Mapato nayo iliboreshwa.”
Baada ya hapo, Lumato anasema kampuni nyingi zilikuja zaidi zikiwamo Shell, KUFPEC, Amocco, Dublin, Tanganyika Oil, lakini utafiti wao haukubaini chochote kwa miaka 10 hadi zilipoondoka nchini ilipofika1992.
“Ili kuboresha zaidi utafutaji wa mafuta, masharti yakalegezwa mwaka 1995 na kuvutia kampuni nyingine zaidi. Hivyo, kampuni zaidi zikaanza kuja kwa mfano: Ndovu iliyojikita Kiliwani, Maurl & Prom iliyokwenda Rufiji na Mafia, Petrodel iliyokwenda Kimbiji na Dominion,” anasema.
Mafuta katika kina kirefu cha bahari
Kwa upande wa mafuta kwenye  bahari ya kina kirefu, Lumato anasema utafutaji ulianza mwaka 1999 kwa TPDC kushirikiana na kampuni za nje kufanya utafiti wa awali. Gharama zake, Dola za Marekali 11 milioni, sawa sh13 bilioni zilitumika kufanikisha utafutaji huo.
Vitalu vyote baharini vilivyotangazwa vina wawekezaji na ugunduzi umefanyika kwenye vitalu vingine.”
“Hadi sasa kuna kampuni za kimataifa 18 zimeshajitokeza kwenye utafutaji huo na mikataba ya utafutaji ipo 25. Mikataba ya miaka 11 imegawanyika katika vipindi vitatu vya miaka minne na mikataba ya kugawana mapato (Production Sharing Agreement – PSA).”
Anaendelea kusema kuwa, utafiti pia umeelekezwa kwenye mabonde ya ufa kama vile Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa,  Ziwa Nyasa, Wembere, Ruhuhu, Bagamoyo na Ruvu, Pangani, Mikumi, Kilosa na Morogoro.
“Mpaka sasa kuna dalili za awali nzuri za upatikanaji wa mafuta. Serikali haigharimii wakati wa utafutaji na hata mafuta yakipatikana mkataba unakuwa na uendelezaji na uzalishaji hadi miaka 45,” anasema.
Uzoefu wa Nigeria
Nigeria ina hazina kubwa ya mafuta katika bara la Afrika ambayo husafirishwa duniani kote. Hata hivyo, nchi hiyo haijaweza kuwaletea wananchi wake hali bora ya maisha. Kwa sasa, nchi hiyo ndiyo ya kwanza kiuchumi barani Afrika.
Asilimia 80 ya pato la taifa nchini humo hutokana na mafuta ghafi. Tangu kuanza kwa uzalishaji wa mafuta hapo mwaka 1958 nchi hiyo imepanda juu na kushika nafasi ya nane duniani kwa kusafirisha mafuta  nje kwa wingi.
Nigeria inazalisha mafuta mapipa milioni 2.6 ya mafuta kwa siku, ni nchi inayozalisha mafuta kwa wingi barani Afrika na ni nchi ya sita ya kusafirisha mafuta kwa nchi za nje duniani. Moja ya tano ya mafuta yanayotumika Marekani yanatoka Nigeria.
Sehemu ya Delta ya Niger, kusini mwa Nigeria ni sehemu muhimu kwa uzalishaji wa mafuta na gesi nchini humo, ambapo karibu mafuta yote na gesi yote yanazalishwa huko, mapato zaidi ya asilimia 90 ya Nigeria yanapatikana kutoka huko.
Mwaka 2010 Nigeria iliuza mafuta  yenye thamani ya Dola 64.4 bilioni kwa Marekani, India, Brazil, Hispania, Uholanzi, Ufaransa, Afrika Kusini, Canada, Ujerumani, Ureno, Ivory Coast, Italia, Ghana, Uingereza na nchi nyinginezo.
Lakini, utajiri wa mafuta na gesi haujawahi kuwaletea wananchi wake manufaa yoyote.
Kinyume chake, migogoro haikuwahi kusimama kati ya makabila na mashirika katika mapambano ya kugombea haki ya kusimamia maliasili ya mafuta na gesi. Kutokana na takwimu, watu zaidi ya 1000 wanakufa kila mwaka katika migogoro ya kutumia silaha katika sehemu ya delta ya Niger.
Kundi maarufu linalotishia usalama katika eneo hilo ni la The Movement for the Emancipation of the Niger Delta.
Hivi karibuni, kundi hilo limetishia kufanya mashambulizi kwenye visima vya mafuta vya shirika la Total la Ufaransa na Agip la Italia na litashambulia kisima cha Chevron ya Marekani.
Kutokana na msukosuko wa muda mrefu, maendeleo ya uchumi na jamii kwenye sehemu hiyo yanaathiriwa vibaya na imekuwa sehemu iliyo nyuma kabisa kiuchumi nchini Nigeria, asilimia 70 ya watu wa huko wanaishi chini ya mstari wa umaskini kabisa. Wakazi wa huko mara kwa mara wanafanya mashambulizi ya silaha kwa mashirika ya nchi za nje yanayochimba mafuta na kuharibu mazingira.
Licha ya eneo hilo kuzalisha mafuta nchini humo, taarifa zinaonyesha kuwa hupewa kiasi kidogo cha bajeti ya serikali hali inayotajwa kuwa chanzo muhimu cha kusababisha mashambulizi ya silaha.
Nyingine ni njia iliyotumiwa na mashirika ya nchi za magharibi yaliyochukua hatua mbalimbali ili kuvutia na kufarakanisha nguvu za aina mbalimbali za wenyeji. Hatua hizo zimechangia kupata nguvu kwa kikundi haramu chenye silaha na mwishowe hatua hizo zimeleta matokeo ya “kujipalia moto”.
Mazingira ya eneo hilo pia yamechafuliwa na shughuli za uchakataji wa mafuta.
Katika mahojiano na Voice of America Dk Innocent Masi kutoka Omoko, kaskazini mwa Port Harcourt ambao ni mji mkubwa kabisa wa jimbo la Niger Delta anasema: “Kiwango cha gesi kinachounguzwa hapa ni cha juu sana. Kumekuwepo na magonjwa ya ngozi yanayohusiana na gesi. Uzazi wa wanawake hapa sio mkubwa kulinganishwa na maeneo mengine.
Mapaa ya nyumba yameathirika, hayadumu kwa muda mrefu. Kama daktari mwenye ujuzi nimegunduwa mabadiliko mengi.”
Haya ni madhara ambayo nchi yetu inawezana kukumbana nayo kama haitajianda vizuri na upatikanaji wa mafuta.
Mafuta na Muungano
Kwa upande wa Zanzibar, nayo haiko nyuma. Hivi karibuni Serikali ya Mapinduzi  (SMZ)  na Kampuni ya Mafuta ya Shell ya Uholanzi zimetia saini makubaliano ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi.
Makubaliano hayo yametiwa saini Agosti28, 2013 mjini The Hague ambapo Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Ramadhani Abdalla Shaaban alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya SMZ na  mwakilishi wa Kampuni Shell Tanzania, Axel Knospe.
Makubaliano hayo yamefikiwa The Hague, Uholanzi wakati wa ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed inayoendelea nchini humo.
Kumekuwa na madai ya wasiwasi wa Zanzibar kutonufaika na rasilimali hiyo kutokana na Muungano kati yake na Tanganyika. Wanasiasa wengi hasa wa Zanzibar wamekuwa wakidai suala la mafuta kuondolewa kwenye mambo ya muungano.
Katika Rasimu ya kwanza naya pili ya Katiba inayoendelea kujadiliwa kabla ya kupatikana kwa Katiba Mpya, suala la gesi na mafuta limeondolewa katika Mambo ya Muungano.
Tanzania inaelekea wapi?
Akizungumzia mwelekeo wa Tanzania katika utafutaji wa mafuta, mwanadiplomasia mkongwe, Dk Ahmed Kiwanuka anasema kuwa ni wazi Tanzania itakuwa kiuchumi kutokana na ongezeko la mapato.
Hata hivyo, Dk Kiwanuka anasema kuwa nchi tajiri zitakuja kwa kasi kuwekeza ikiwa pamoja na kusaini mikataba ya ulaghai.
“Kupatikana kwa mafuta Tanzania ni ishara kukua kwa uchumi kimataifa. Hapo ni lazima nchi tajiri zije kupambana kupata mafuta hayo ni iwe ni kwa mikataba halali au haramu. Wao hawajali, hata nchi iingie vitani, wanachojali ni kufaidika na mafuta,” anasema Dk Kiwanuka
Anasema ili Tanzania iepukane na machafuko ya ndani au na nchi jirani, ni lazima kuwe na viongozi waadilifu:
“Tusipokuwa waangalifu lazima tupigane na nchi jirani, kama ilivyo kwa Malawi sasa. Lakini, hatuna sababu ya kugombana, tujifunze kwa nchi za Ufaransa na Ujerumani ambazo ziligombana kutokana na rasilimali zilizokuwa mipakani miaka ya 1940. Lakini baadaye zimeungana na kugawana mapato,” anasema na kuongeza:
“Siyo hizo tu, nchi za Ulaya zimeungana na sasa zina umoja wao wa Ulaya. Wanashirikiana kiuchumi na kijamii ndiyo maana wana nguvu. Sisi na Malawi kwa nini tugombane? Tunaweza kuitumia Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kusuluhisha na tukasonga mbele,” anasema.
Anaendelea: “Naamini Rais wa Malawi, Profesa Peter Mutharika ni mwanasheria mzuri, hivyo atatumia busara katika mgogoro huu.”
Kwa upande wake,  Dk Wetengere Kitojo japo anasema mzozo kati ya Tanzania na Malawi haukuanzishwa na utafutaji wa mafuta, unaweza kukua kutoka na rasilimali hiyo.
“Chanzo cha mgogoro kati ya Tanzania siyo utafutaji wa mafuta, bali ulikuwepo tangu miaka ya nyuma enzi za ukoloni wa Mwingereza. Kwa sasa umeibuka tu kutokana na utafutaji wa mafuta. Ni kawaida kutokea mizozo hiyo hasa rasilimali zinapogundulika mipakani,” anasema Dk. Kitojo na kuongeza:
“Kidiplomasia hili ni suala la pande mbili kukaa na kujadiliana. Siwezi kutabiri mazungumzo yanayoendelea, lakini naamini Rais Profesa Mutharika atakuwa mwelewa.”
Akifafanua hali ya mgogoro wa kugombea mpaka wa  Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi, Balozi wa Tanzania nchini humo, Patrick Tsere anasema kwa sasa uko mikononi mwa msuluhishi ambaye ni Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano.
Chissano ambaye pia ni mwenyekiti wa jopo la marais wastaafu wa Afrika anasaidiwa pia na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Festus Mogae wa Botswana.
“Kikao cha kwanza kilifanyika  Mach 2014, mjini Maputo na kikao kijacho kiilikuwa kifanyike baada ya uchaguzi nchini Malawi. Kama siyo Juni, basi  baadae Julai 2014,” anasema Balozi Tsere.
Kuhusu kauli za Rais Mutharika katika mgogoro huo, Tsere anasema:
“Yale matamshi aliyoyatoa kwamba ziwa lote ni lao, aliyatoa akiwa hajawa Rais na bila ya shaka mwingine yoyote angesema kama alivyosema Mutharika, hasa ukichukulia kilikuwa ni kipindi ambacho alikuwa hajaingia madarakani,” anasema na kuongeza:
“Sasa baada ya kuingia madarakani atakuwa amepata fursa ya kufahamu kila kitu kinachohusiana na suala hili na bila shaka kumsaidia kufanya uamuzi wa kuendelea kushiriki kwenye mazungumzo.
Kumbuka suala hili la mazungumzo alilianzisha marehemu kaka yake akiwa Rais, alipomuomba Rais Mkapa, Juni 2005 juu ya umuhimu wa kukaa pamoja na kulimaliza suala hili. Pili, yeye ni mwanasheria na ni msomi ni vizuri aepuke hisia za kisiasa na aliangalie suala hilo kwa macho yanayostahili.”
Balozi Tsere anajipa moyo kwamba, kwa kuwa hata Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pia ni mwanasheria ambaye aliwahi kufanya kazi nchini , shirika la wakimbizi (UNHCR)  hukoNgara mwishoni mwa miaka ya ‘90, hivyo atakuwa mwelewa katika suala hilo.
CHANZO. MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...



aziz bilal06:27


1
Reply

Kitakachofuatia ni vita ya wenyewe kwa wenyewe ya kugombania mali

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!