RAIS Barack Obama wa Marekani amesema ni mapema sana kupeleka dawa ya majaribio ya ugonjwa wa ebola Magharibi mwa Afrika, ingawa Liberia imetangaza hali ya hatari nchini humo kutokana na kusambaa kwa ugonjwa huo ambao hauoneshi dalili za kupungua.
Obama alisema kutopeleka dawa hiyo ya majaribio kunatokana na kukosekana kwa taarifa kamili juu ya dawa hiyo ya ZMapp ambayo walipewa wataalamu wawili wa afya wa Wamarekani, waliopata maambukizi ya ugonjwa huo nchini Liberia walikokuwa wakisaidia utoaji huduma na kupata ahueni.
“Tuache sayansi ituongoze, sidhani kama tuna taarifa kamili iwapo dawa hiyo ni msaada kwetu, virusi vya ebola tangu zamani vinaweza kuzuilika tu kama tuna miundombinu ya tiba imara kwenye maeneo yetu,” alisema Obama na kuongeza ataendelea kufuatilia taarifa za dawa hiyo.
Kauli hiyo ya Rais Obama imekuja siku chache baada ya wataalamu wa masuala ya ebola kuhoji kwa nini wafanyakazi wa afya wa Marekani ndio pekee waliopewa dawa za majaribio ambapo kampuni husika imedai dawa hizo ni chache.
Wataalamu watatu wa masuala hayo walitaka dawa hizo za majaribio na chanjo zipewe kwa watu wa Afrika Magharibi ambao ndio wamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo hatari unaoua kwa kasi.
Wataalamu hao akiwemo Peter Piot, aliyegundua ebola mwaka 1976 alisema Waafrika walioathirika na ugonjwa huo wanatakiwa kupewa fursa kama walizopewa Wamarekani hao.
“Shirika la Afya Duniani (WHO), chombo pekee chenye mamlaka ya kimataifa kuruhusu majaribio ya tiba kinapaswa kuongoza katika hili,” alisema.
Karibu watu 900 kutoka nchini Guinea, Sierra Leone, Liberia na Nigeria wamekufa kwa ebola na wengine zaidi ya 1,600 wamepata maambukizi tangu virusi vya ugonjwa huo viliposambaa Guinea Februari, mwaka huu.
HABARI LEO.
HABARI LEO.
No comments:
Post a Comment