Tuesday, 5 August 2014

MLEMAVU MBARONI KWA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA




JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linamshikilia Said Tidwa (36), mkazi wa , Temeke kwa tuhuma za kufanya biashara ya dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda Maalum, Kamishna Suleiman Kova, alisema taarifa za kiintelijensia zilizopatikana kutoka kwa raia wema ziliwafikia makachero wa polisi kuwa Tidwa ambaye ni mlemavu wa mguu anajihusisha na biashara hiyo.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, mtuhumiwa huyo ana mguu wa bandia anaoutumia kuficha dawa hizo na kuziuza rejareja kwa wateja wake ambapo kila kete huuza sh. 1,000.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba mtuhumiwa huyo anatumia mbinu hiyo kwa muda mrefu kabla ya kukamatwa Agosti Mosi, mwaka huu,” alisema Kova na kuzitaja dawa alizokutwa nazo kuwa ni cocaine, heroine na wakati mwingine bangi.
“Natoa onyo kwa watu wenye ulemavu, wasitumie kigezo cha ulemavu kufanya uhalifu kwa makusudi kwani wanaharibia walemavu wengine ambao ni raia wema ambao sio rahisi kuwatilia shaka,” alisisitiza kamanda huyo.
Wakati huo huo, wanawake watatu wamekamatwa na jeshi hilo akiwemo mwanafunzi wa Chuo cha Genessis kilichopo Mtoni kwa Azizi Ali, Stela Daniel (17) kwa kujihusisha na mtandao wa wezi wa nyara za serikali.
Kamanda Kova aliwataja wengine kuwa ni Wemael Mshana na Upendo Mshana (33) waliokamatwa Julai 23 huko Mbagala Mission wakiwa na vipande sita vya meno ya tembo yenye thamani ya sh. milioni 49.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo linamshikilia Venance Manyika (38), Mkazi wa Mbagala Mission kwa kosa la kukutwa na ngozi ya chui kinyume na sheria.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 29 mwaka huu huko Mbagala Mission na askari waliokuwa katika msako wa kupambana na uhalifu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!