Wednesday 6 August 2014

MAWAZIRI SADC KUJADILI EBOLA


MAWAZIRI wa Afya na wadau wengine wa afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC), leo wanakutana kwenye mkutano wa dharura kuzungumzia hatua za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.


Mkutano huo unafanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini una lengo la kutoka na maazimio ya pamoja ya jinsi ya kukabili mlipuko wa ugonjwa huo ulioenea Magharibi mwa Afrika ambao umeua mamia ya watu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki mkutano huo ikiwakilishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Steven Kebwe ambaye ameshawasili nchini humo.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja alisema Naibu Waziri atakaporejea nchini, atatoa taarifa ya yaliyojiri na hatua walizoafikiana kuchukua kuthibiti ugonjwa huo.
“Ni kweli kuna mkutano huo, na sisi kama wanachama wa SADC, tunahudhuria, Naibu Waziri tayari yupo huko akirejea tutautaarifu umma yaliyojiri,” alisema Mwamwaja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sekretarieti ya SADC, mkutano huo wa dharura, unafanyika leo jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Shirika la Afya Duniani (WHO), na wadau wengine wanashiriki. “Lengo la mkutano huo ni kuja na nguvu ya pamoja ya nini cha kufanya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo, ambao unaendelea kuangamiza maisha ya watu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema mkutano huo, utatoka pia na maazimio ya pamoja ya mawaziri hao jinsi ya kudhibiti ukanda wa SADC, dhidi ya ugonjwa huo.
Ugonjwa huo usio na tiba wala chanjo hadi sasa umekumba nchi za Guinea, Liberia, Sierre Leone na Nigeria. Umesababisha vifo vya zaidi ya watu 800 wakiwemo pia wataalamu na watafiti wa ugonjwa huo.
Hivi karibuni, serikali ilitoa hadhari kuhusu ugonjwa huo na kusema imesambaza wataalamu wake kwenye mipaka nchi nzima kuukabili endapo utaibuka. Alisema wataalamu wa afya wataendelea kutoa elimu ya afya juu ya ugonjwa huo ambao haujaripotiwa kuingia nchini.
Dalili za ugonjwa wa Ebola ni pamoja na homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na kupatwa na vidonda kooni.
Baada ya dalili hizo mgonjwa hutapika, kuharisha, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na vipele mwilini na kutokwa na damu sehemu zote mwilini zenye matundu na mwisho ni kifo.
Dalili hizo huonekana baada ya siku mbili hadi 21, ya mtu kupatwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.
Wakati huohuo Benki ya Dunia imetangaza kutoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 200 za dharura kwa ajili ya kuzisaidia nchi za Afrika Magharibi ambazo zimekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya Ebola.
Fedha hizo zitasambazwa kwa Serikali za Liberia, Sierra Leone na Guinea pamoja na Shirika la Afya Dunaini (WHO).
Ripoti za WHO zinaonesha kuwa idadi ya watu ambao wamepoteza maisha kutokana na maradhi hayo hatari ni 887.
Tangazo hilo limefanywa na Benki ya Dunia wakati wa mkutano unaowahusisha viongozi wa nchi za Afrika na Marekani ambao unaendelea mjini Washington ambao unajadili masuala mbalimbali.
Rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim, alisema amehuzunishwa na mlipuko huo wa Ebola ambao umesababisha mfumo wa afya wa nchi hizo tatu kuzorota kutokana na kutokuwa na uwezo kifedha kukabiliana na maradhi hayo.
"Nina wasiwasi kwamba watu wengine zaidi wako kwenye hatari ya kuambukizwa ebola, hivyo ni lazima tusaidie kupunguza maambukizi haya," alisema.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Paul Blake, alisema fedha hizo ambazo zitatolewa katika mpango wa kipindi kifupi zitasaidia kuwalipa wafanyakazi wanaowahudumia wagonjwa wa Ebola, ujenzi wa vituo na usambazaji wa dawa kwa wagonjwa wa vijijini na kutoa elimu ya kuwapeleka wagonjwa haraka kwenye vituo vya afya.
Chini ya mpango wa muda mrefu, fedha hizo pia zitasaidia nchi hizo ziweze kujikwamua kiuchumi kutokana na matatizo yaliyosabishwa na maradhi ya Ebola.
Fungu hilo sasa linasubiri kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo na taarifa zinadai kuwa uidhinishwaji huo unaweza kufanywa wiki hii. Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) walisema utafiti unaonesha kwamba kusambaa kwa maradhi hayo kutaathiri zaidi uchumi wa nchi hizo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!