Thursday, 21 August 2014

HILONDILO JIBU LA HOJA URAIA PACHA!

Tanzania Diaspora Initiative
MIMI si mmoja wa watu wanaoamini katika pendekezo kuwa Katiba mpya iweke ndani kipengele cha kutambua uraia wa nchi mbili au kama wengine wanavyouita “uraia pacha”.

Kumekuwepo na wanaharakati na Watanzania wengine ambao wanaamini kabisa kuwa uraia wa nchi mbili ni jambo ambalo linastahili kuingizwa kwenye Katiba mpya.
Wengi wanaozungumzia suala hili la uraia wa nchi mbili wanazungumzia hasa faida zake hasa kwa watu ambao wanataka kuja kuwekeza Tanzania kama Watanzania na si wageni.
Wapo wengine wanaozungumzia suala hili kwa misingi hasa ya kile kinachoitwa “faida za kiuchumi” za uraia wa nchi mbili. Lakini kabla ya kuangalia kwa undani kidogo na kusoma suluhisho langu (ambalo labda wengine wamelitoa pia) juu ya suala niangalize mambo yafuatayo.
Uraia wa pacha ni nini?
Kimsingi ni ile hali ya mtu kuwa raia wa nchi mbili wakati mmoja. Mtu anaweza kuwa raia wa Tanzania na wakati huo huo akawa raia wa Marekani kwa mfano. Hata hivyo ukiangalia maneno yenyewe hayako sawa vile vile; kwanini tunazungumzia haki ya kuwa raia wa “nchi mbili” lakini siyo haki ya kuwa raia wa “nchi tatu” au zaidi?
Kwanini hoja iwe ni “uraia wa nchi mbili” kwani ni lazima ziwe nchi mbili ndio mwisho? Itakuwaje kama mtu kutokana na sababu mbalimbali anataka kuwa na uraia wa Tanzania, Kenya na Uingereza?
Hivyo, naamini la kuanza ni kusahihisha maneno haya; tunachozungumzia hasa ni ile haki ya mtu kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja. Na ninachozungumzia mimi hapa ni hili hasa siyo suala tu la uraia wa nchi mbili bali suala la uraia wa nchi zaidi ya moja. Tukizungumza hivi tunaweza kuelewana vizuri.
Ni wazi kuwa watu wengi wanaweza kuwa na uraia wa nchi mbili na ni wachache wanaweza kuwa na uraia wa zaidi ya nchi hizo mbili na labda kwa minajili hiyo ndio maana watu wanazungumzia sana uraia wa nchi mbili.
Hili nalielewa na kwa ajili ya mjadala wetu hapa tuendelee na dhana au nadharia hii ya “nchi mbili” lakini ijulikane tunazungumzia pia kwa zaidi ya nchi mbili.
Kwanini Tanzania haina uraia pacha?
Mojawapo ya mambo ambayo hatujayasikia sana na hayajafafanuliwa vizuri ni kwanini Tanzania haikuruhusu au hairuhusu uraia wa nchi mbili. Ni vizuri turudi nyuma kidogo na kukumbushana historia ya kwanini suala la uraia wa zaidi ya nchi moja lilikataliwa na kwanini ninaamini katazo hilo bado lina hoja ya nguvu lakini pia ni msingi wa kuweza kutatua tatizo hili – kama tunaweza kuliita ni tatizo.
Wakati tunaelekea uhuru na mara baada ya uhuru hoja ya suala la uraia ilikuwepo katika jamii yetu; na hapa nazungumzia Tanganyika. Tukumbuke kuwa hadi tunafikia uhuru tayari nchini yetu ilikuwa na watu wengi tu walioishi na kufanya makazi yao Tanganyika wao wenyewe wakiwa na asili ya nje ya bara la Afrika. Walikuwepo Wahindi, Washirazi, Waarabu ambao wengine walishaishi hapa kwa vizazi na wengine wakiwa wahamiaji wa siku za karibuni.
Swali kubwa lilikuwa ni je tukipata uhuru ni nani atakuwa raia wa Tanganyika na kwanini. Kulikuwa na kambi mbili kubwa na zilizokuwa zinaamini zina hoja sana. Moja ilikuwa ni kambi ya wale walioamini kuwa uraia ulitakiwa uwe wa Waafrika weusi tu (Watanganyika) wakati wengine waombe au kuwa na sifa nyingine lakini wasipewe uraia moja kwa moja.
Kambi ya pili – ambayo iliongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere ilikuwa inaamini katika nadharia ambayo nitaifafanua hapa chini na ambayo ndio msingi wa kwanini uraia wa nchi mbili ulikataliwa miaka zaidi ya hamsini iliyopita.
Kambi hizi mbili zilijikuta zinapambana kwenye Baraza la Kutunga Sheria (Bunge) miezi kama miwili tu kabla ya Tanganyika kupata uhuru. Serikali ilikuwa imeandaa waraka wenye kutoa mwongozo wa kuelekea utungaji wa sheria ya uraia kabla tu Tanganyika haijapata uhuru. Mjadala bungeni ulikuwa unahusiana na waraka huo na muswada wa sheria ya uraia wa Tanganyika.        
Baadhi ya wazungumzaji waliozungumza kabla ya Nyerere walishangiliwa walipotetea hoja ya “Uafrika” kama msingi wa uraia. Huu “uafrika” walikuwa wanamaanisha hasa ni “weusi” kwamba wale Watanganyika “weusi” ndio watakuwa raia na wengine watafikiria baadaye na watachukuliwa kama wageni. Ilionekana kuna kundi kubwa tu lililounga mkono mawazo haya na tukiangalia vizuri historia tunaona kundi hili lilikuwa na nguvu hata miaka michache baadaye kwa kulazimisha ile sera ya “africanization” ya utumishi wa umma.
Nyerere aliwasikiliza kwa makini huku akionekana wazi mwenye hasira. Ilipofika zamu yake kujibu hoja mbalimbali – wakati huo alikuwa ni Waziri Mkuu – alizungumza kwa hisia kali na alitoa mojawapo ya hotuba zake maarufu sana. Nyerere alizungumza akijenga hoja ni kitu gani kitakuwa ndiyo ‘kanuni’ ya uraia kwa Tanganyika.
Kanuni ya uraia iliyoondoa uraia pacha
Nyerere alianza kwa kuuliza maswali mawili na kuyajibu. “Sasa waheshimiwa sisi tunajaribu kufanya nini? Aliuliza. Akajibu, “tunatengeneza  uraia wa Tanganyika”. Hili lilikuwa swali la kwanza. Hapo hapo akafuatia na swali la pili “Ni nini kitakuwa msingi wa uraia huo wa Tanganyika?” na hili akalijibu; “Sisi, katika Serikali, tuliochaguliwa na Watanganyika tunasema utii kwa nchi yetu ndio utakuwa msingi wa kuamua uraia wa nchi yetu”.
Kutoka hapo Nyerere alishambulia hoja za “uafrika” kama msingi wa uraia bila huruma; hakumung’unya maneno na alizungumza bila kuandika hotuba. Waliozungumza kabla yake walidai wanafanya hivyo wakiwakilisha Watanganyika na yeye alisema kwenye hili atakuwa mtu wa demokrasia kweli kweli.
Kama kweli Watanganyika wanataka rangi kuwa msingi wa uraia basi ipigwe kura na itakuwa ya siri kabisa na huru (bila kutumia nyezo za chama). Alisema wazi kabisa kuwa endapo kura ingeonesha kuwa wanaotaka rangi ya mtu kuwa kigezo cha uraia basi yeye na serikali yake watajiuzulu mara moja.
Alisema ‘let the representatives here of the people of Tanganyika reject shis Motion and we shall resign immediately, and I mean it.” Kwamba, “basi wawakilishi wa wananchi hapa waikatae hoja yetu na wakiikataa sisi tutajiuzulu mara moja, na ninamaanisha hili’.
Kimsingi kabisa, hoja yake na hoja ya serikali aliyoongoza ilikuwa sahihi sana; kwamba uraia hauwezi kuamuliwa kwa kuangalia kitu kingine chochote isipokuwa utii (loyalty) kwa nchi.
Huwezi kuamua uraia kwa kuangalia faida za kiuchumi, au kitu kingine kwani ukifanya hiyvo utajikuta unapata shida mara moja. Wanaozungumzia faida za kiuchumi kwa mfano wanazungumza wakimaanisha wale Watanzania wanaoishi kwenye nchi zilizoendelea; vipi kwa Watanzania ambao wanaishi kwenye nchi nyingine maskini au jirani zetu wao watafaidika vipi kiuchumi?
Itaendele wiki ijayo…
TZ-DAIMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!