Pages

Friday, 25 July 2014

ZIJUE FAIDA ZA TIKITI MAJI

Tikitimaji
TIKITIMAJI ni kati ya tunda linaloonekana kupendwa na watu wengi katika miaka ya hivi karibuni.
Sababu ya kupendwa ni kutokana na utamu wake na maji ambayo yanapatikana kiasi kwamba kama una kiu unaweza kuahirisha kunywa maji.

Mtaalamu wa tiba asili, Abdallah Mandai, anasema tikitimaji ni kati ya tunda  lenye virutubisho mbalimbali vyenye faida kubwa katika afya ya binadamu.
Mandai anasema licha ya tikiti kuwa na maji asilimia 92, asilimia nane zilizobaki zina faida kubwa kiafya, jambo linaloonekana kutofahamika kwa wengi.
Chanzo cha vitamini
Mandai anasema katika tunda hilo lina Vitamin A, inayosaidia kuboresha afya ya macho na pia kuondosha sumu mwilini, Vitamin C, inayosaidia kuboresha kinga, kuponya majeraha, kukinga uharifu wa seli, kuboresha afya meno na fizi na vitamini B6, inayosaidia ubongo kufanya kazi na kuibadilisha protini kuwa nishati.
“Tikitimaji lina kiwango kikubwa cha lycopene kuliko tunda lolote au mboga za majani. Ikiwa familia yako inaishi kwenye eneo lisilo na vyanzo vya madini ya potasium, unaweza kuwapa tikiti badala yake ambalo lina uwezo wa kusaidia misuli na mfumo wa fahamu kwa ujumla kufanya kazi zake vizuri,” anasema mtabibu huyo.
Pia anasema tunda hilo lina Amino asidi na virutubisho vingine vinavyosaidia kurahisisha mtiririko wa damu kwenye mishipa yake.
Anasema ulaji wa kipande kimoja cha tikitimaji baada ya mazoezi makali, husaidia kuondoa tatizo la kukaza kwa misuli ya miguu.
Sifa nyingine iliyopo katika tunda hili, ni uwezo wake wa kusaidia kupunguza ama kuondoa tatizo la upungufu wa nguvu za kiume na kwamba mnywaji atatakiwa kunywa juisi ya tunda hilo iliyokamuliwa bila kumenywa maganda.
Pia anasema tikiti husaidia kupunguza uzito mwilini, kwani  lina kiwango kidogo cha kalori.
“Kwa mtu anayetaka kupunguza uzito wa mwili linaweza kumsaidia kwa kula kwa wingi. Atakuwa anajisikia tumbo kujaa, lakini bila kuwa ameshiba, hivyo kuwa rahisi kwake kujizuia kula vyakula vingine na bila kuathirika kiafya,” anasema.
Anaeleza kirutubisho kinachojulikana kwa jina la ‘Arginine’ kilichomo kwenye Tikitimaji kina kazi nyingi mwilini ambako  huchochea kwa kiasi kikubwa uimarishaji wa kinga ya mwili.
Kazi ingine ya tunda hilo kirutubisho hicho cha ‘Arginine’, ni kusaidia kuponyesha vidonda na kuondoa sumu nyingine mwilini ambazo zinapozidi humfanya mtu kusikia uchovu na kusababisha ugonjwa wa ini na figo.
Faida nyingine za tikitimaji ni kushusha shinikizo la juu la damu, huongeza nuru ya macho, hutoa kinga kubwa dhidi ya magonjwa nyemelezi yakiwemo yale hatari kama kansa ya matiti, kibofu cha mkojo, mapafu na kansa ya tumbo.
Hivyo, anashauri  watu kutumia tunda hili mara kwa mara wakati yu mzima, ili kuupa kinga mwili na kumuepusha na maradhi nyemelezi, kwani kinga ni bora kuliko tiba

No comments:

Post a Comment