Pages

Wednesday, 30 July 2014

WATANZANIA WATATU MBARONI KWA KUINGIA NCHINI KINYUME CHA SHERIA-KENYA

 
Watanzania watatu wanashikiliwa nchini Kenya kwa kosa la kuingia nchini humo kinyume cha sheria na kuhusishwa na matukio kadhaa ya kigaidi yaliyotokea nchini humo.

Watu hao waliokamatwa mjini Lamu Alhamisi iliyopita na kupelekwa Nairobi, watafikishwa mahakamani kesho kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu alisema Watanzania hao wanakabiliwa na kosa la uhamiaji haramu na kuingia nchini humo bila kufuata taratibu.
“Watanzania hawa wanakabiliwa na mashtaka ya kuingia nchini Kenya bila kufuata taratibu. Taarifa za kuwa wanahusika na ugaidi siyo za kweli na hazijathibitika,” alisema Mngulu na kuwataka Watanzania wengine kufuata taratibu pindi wanapovuka mipaka ya nchi.
Mngulu alisema sheria ya kimataifa inaruhusu mtuhumiwa yeyote kushtakiwa katika eneo alikotenda kosa bila kujali uraia wake.
Alibainisha kuwa wakati mwingine nchi inaweza ikaomba raia wake washtakiwe nyumbani endapo kutakuwa na makubaliano baina ya nchi mbili zinazohusika.
Ripoti kutoka Kenya zinasema watuhumiwa wawili kati yao walikutwa na pasi za kusafiria zilizokwisha muda wake.
Gazeti la The Star la nchini humo liliripoti kuwa polisi walipekua simu za watuhumiwa hao na kubaini kuwa walikuwa na mawasiliano ya karibu na Al-Shabaab.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment