Pages

Monday, 28 July 2014

WATALII 17 WAVAMIWA HOTELINI

Weruweru River Lodge
KUNDI la watu wanaoaminika kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za moto na mapanga, wamevamia watalii 17 kutoka mataifa mbalimbali na kuwapora kiasi kikubwa cha fedha, kamera na kompyuta mpakato (Laptop), kisha kuwajeruhi wanne na kutoweka.

Tukio hilo kubwa kuwahi kutokea siku za hivi karibuni mkoani Kilimanjaro, limetokea juzi alifajiri eneo la Mailisita kwenye hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge inayomilikiwa na mfanyabiashara Cuthbert Swai, ambaye pia anamiliki kampuni ya wakala wa utalii ya Ahsante Tours ya mjini hapa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, watalii hao kutoka mataifa mbalimbali, walikumbwa na mkasa huo wakiwa wamelala ndani ya mahema majira ya saa 9 alfajiri, ambako walitishwa kwa bunduki na mapanga kabla ya kuporwa mali zao.
Katika tukio hilo, watalii watatu waliporwa zaidi ya dola 2,090 za Marekani, mmoja pauni 110 za Uingereza na euro kiasi kisichojulikana, sh milioni 5.4, kamera zaidi ya nne na moja ikiwa na thamani ya sh milioni 1.5 na nyingine ikiwa na thamani ya dola 3,000 za Marekani, zaidi ya sh milioni 4.5.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizothibitishwa na Kamanda wa Mkoa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Robert Boaz, majambazi hao kabla ya kufanya uhalifu huo, waliwakusanya watalii hao eneo moja na kuanza kuwapora kila kitu walichokuwa nacho.
Hata hivyo, Kamanda Boaz hakuweza kulizungumzia tukio hilo kwa kina, ikiwamo kutaja majina ya watalii hao, uraia wao na thamani halisi ya mali walizoporwa, kutokana na kuwa katika pilikapilika za kwenda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kupokea ugeni wa Spika wa Bunge la Nigeria.
Kamanda Boaz, aliwaambia waandishi wa habari waliofika ofisini kwake jana kuwa tukio hilo atalitolea maelezo kamili leo kutokana na kutingwa na ugeni huo.
Ofisa mmoja wa polisi aliyeomba kutotajwa jina lake, alisema kuwa miongoni mwa watalii hao walioporwa mali zao, wako wanne waliokuwa wakijiandaa kuondoka na ndege alfajiri hiyo kupitia KIA.
Aliongeza kuwa watalii hao walijikuta katika mkasa huo, baada ya dereva wa gari lililokuwa limewabeba kuwashwa kuashiria kuondoka hotelini hapo, ndipo majambazi hao walipolivamia na kuanza kuwashambulia na hatimaye kuwapora mali zao ingawa watalii hao waliendelea na safari yao.
Mmoja wa wakurugenzi wa hoteli hiyo, Stella Shangali alipoulizwa juu ya tukio hilo, hakukiri wala kukanusha kuwapo, zaidi ya kumtaka mwandishi kuwasiliana na kamanda wa mkoa kwa ufafanuzi zaidi.
KWA HISANI YA TZ-DAIMA

No comments:

Post a Comment