Pages

Thursday, 24 July 2014

SIPENDI KUSUTWA-KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete (katikati) akikata utepe, wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kutoka Tunduru mkoani Ruvuma kwenda Mangaka mkoa jirani wa Mtwara. Barabara hiyo itajengwa na kampuni ya Synohydro kutoka China. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Balozi mdogo wa Japan, Kazuyoshi Matsunanga,Waziri wa Ujenzi John Magufuli na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho (kulia).

RAIS Jakaya Kikwete amesema ametimiza ahadi zake kwa wananchi, kwa kuwa hapendi kusutwa.
Amesema miongoni mwa ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, ni ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, ikiwemo barabara.



Aliwaambia wananchi wilayani hapa, kwamba anajivunia kwa mafanikio yaliyopatikana kwenye eneo hilo. Kwa mujibu wake, katika mwaka huu wa fedha, Mfuko wa Barabara umepewa Sh bilioni 726. Alisema kwanza zitajengwa barabara kuu.
“Sipendi nikiondoka watu wanisute ooh mzee muongo,” alisema Rais Kikwete wakati anahutubia mamia ya wananchi mjini Namtumbo, baada ya kufungua barabara ya Songea- Namtumbo.
Licha ya kuzindua barabara hiyo, yenye urefu wa kilometa 71.4, Rais Kikwete aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Namtumbo-Kilimasera- Matemanga, yenye urefu wa kilometa 128.9.
Alisema aliahidi kujengwa kwa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo, imejengwa na ameifungua. Alisema pia wodi ya kinamama hospitalini hapo itaboreshwa.
Kwa mujibu wake, wakati anahutubia wananchi wa Tunduru wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2005, aliahidi barabara ya Tunduru- Matemanga- Mangaka itajengwa; ahadi ambayo sasa inatekelezwa.
“Hivi nisingetekeleza, mwakani wakati napita kumnadi mgombea wa CCM ningeficha wapi sura yangu?” Alihoji na kusema wapo watu hawakuamini kama barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami.
“Watafute uongo mwingine, barabara hii itakamilika,” alisema Rais Kikwete kwenye mkutano huo, uliohudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali.
Miongoni mwa waliohudhuria ni mawaziri, watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Balozi Mdogo wa Japan nchini, Kazuyoshi Matsunanga na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Tonia Kandiero.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, barabara zenye urefu wa kilomita 11,574 zinajengwa kote nchini. Wazembe wafukuzwe Katika uzinduzi huo, Rais aliamuru wakandarasi wazembe na watakaojenga chini ya kiwango, wafukuzwe kuhakikisha kabla ya kukabidhi, barabara inakuwa na kiwango kinachostahili.
“Tusipokee barabara iliyojengwa chini ya kiwango,” alisisitiza. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli katika mkutano huo, alisema Rais Kikwete ni mfano wa kuigwa, kwa kuwa ni viongozi wachache duniani wanaotoa ahadi na kuzitekeleza. Magufuli alisema miongoni mwa ahadi alizotoa Rais Kikwete ni amani ambayo ameitimiza. “Tumekusanyika hapa kwa sababu ya amani, ulilitimiza hilo Mheshimiwa Rais kwa sababu wewe umelelewa kwenye amani,” alisema.
Akitoa mfano wa nchi zenye machafuko ikiwemo Syria, Urusi, Libya, Misri, Kenya na Nigeria, Magufuli alisema,“Ulitambua (alimwambia rais) maendeleo yataletwa na amani…ni viongozi wachache humu duniani wanaotoa ahadi na ahadi hizo zinakamilika.”
Dk Magufuli aliahidi kutekeleza kikamilifu agizo la Rais Kikwete la kutowavumilia wakandarasi wazembe na kwamba hayupo tayari kufukuzwa kazi kwa sababu ya uzembe wa wakandarasi.
“Kabla hujanifukuza mimi hawa wataondoka, hawa tutawasimamia… hawa makandarasi wamesikia, hawa makandarasi wamesikia, narudia, hawa makandarasi,” alisema Waziri Magufuli.
Aidha, Magufuli alisema alimuagiza Ofisa Mtendaji Mkuu Tanroads na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, wahakikishe kazi ya usaidizi wakati wa ujenzi zinafanywa na vijana wa Tunduru

HABARI LEO.

No comments:

Post a Comment