Pages

Thursday, 24 July 2014

SAKATA LA VIUNGO VYA MAITI BUNJU MADAKTARI WAIKAANGA IMTU


Rais wa MAT, Dk Primus Saidia
CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) sanjari na hospitali iliyo chini yake, vinastahili kufungiwa.



Tamko hilo la chama limekuja huku mamlaka mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa karibu wa vyuo vikuu vya matibabu zikikiweka chuo hicho kiporo, kusubiri uchunguzi wa tuhuma zinazokikabili za kutupa viungo vya binadamu jalalani, ukamilike kabla ya kuchukua hatua zinazostahili.
Kitendo hicho cha kutupa viungo vya binadamu jalalani kimetajwa na watu mbalimbali, wakiwemo wataalamu kuwa ni cha ajabu kinachodhalilisha nchi na utu wa binadamu.
Chuo kifungiwe
Rais wa MAT, Dk Primus Saidia alisema kitendo hicho ni cha aibu na kwamba kama ingekuwa nchi nyingine, walistahili kufungiwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema taasisi hiyo isingetakiwa kutoa mafunzo ya udaktari wala kufanya tafiti zozote, ikiwa ni pamoja na kutoruhusiwa kutoa huduma za afya katika hospitali yake.
Mwingine aliyezungumzia sakata hilo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Margareth Sitta aliyepongeza taasisi za serikali kwa hatua za haraka walizochukua kuhakikisha watu hao wanabainika mapema na kukamatwa.
Wawekwa kiporo
Hata hivyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa nyakati tofauti, walisisitiza nia yao ya kuchukua hatua dhidi ya chuo hicho, mara jopo linalochunguza sakata hilo litakapokamilisha kazi yake.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen aliliambia gazeti hili kwamba amesikitishwa na kitendo hicho ambacho si cha kawaida. Alitaka upelelezi ufanyike haraka, adhabu stahiki ichukuliwe kutokana na kitendo hicho.
“Baada ya kukamilika kwa upelelezi wa tukio hili na kupata taarifa za kwa nini walifikia hatua hii, naahidi wizara yangu itachukua hatua kali,” alisema Kebwe.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja alisema kutokana na kuwa jambo hilo ni jipya, wataangalia uwezekano wa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema ingawa wizara yake haihusiki na usimamizi wa vyuo hivyo vinavyozalisha madakatri na kutaka waulizwe TCU, kwa mujibu wa Mwamwaja, kitendo walichofanya madaktari husika si cha kimaadili.
Alisema pamoja na kuwa kitendo hicho si cha maadili pia wanaangalia madhara ya kiafya kulingana na tukio hilo.
“Lakini pia ni vema kuangalia na jiji (Dar es Salaam) ni jinsi gani wanasimamia madampo yao, kwa nini inaruhusu kumwaga uchafu wowote bila kuwepo wakaguzi au ni utaratibu gani wanatumia kulinda afya za wananchi,”alisema Mwamwaja.
Sheria inasemaje?
Kwa upande wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yenye dhamana na vyuo vikuu, Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome alisema pia wanasubiri ripoti ya timu iliyoundwa kuchunguza suala hilo wachukue hatua za haraka chini ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
“Kwa sasa uchunguzi unaendelea hivyo hatuwezi kuchukua hatua yoyote,” alisema Profesa Mchome.
Katibu Mkuu alisema katika tume hiyo iliyoundwa na polisi, yumo mwakilishi wa elimu kutoka TCU. Alisisitiza wataangalia suala hilo na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kwa sasa hakuna sheria inayowabana kutokana na kuwa suala hilo ni jipya nchini.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku alisema wanasimamia ubora wa elimu ya juu na suala lililotokea ni kesi ya chuo kwa asilimia 100.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa Mkurugenzi wa Ithibati wa Elimu ya Juu katika tume hiyo yupo kwenye tume iliyoundwa, wataangalia hatua za kuchukua baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema TCU ni taasisi yenye utaratibu, hivyo itatoa uamuzi baada ya ripoti kwa kuwa sasa IMTU bado ni watuhumiwa na haipaswi kuhukumiwa.
“Tunasubiri tume imalize uchunguzi ndipo tutaona tutachukua hatua gani kulingana na Sheria ya Vyuo Vikuu kwani kwa sasa sheria ya suala hilo haipo kutokana na kwamba ni jipya kutokea nchini,”alisema.
Wakili wa Kujitegemea kutoka MK Law Chambers, Karoli Mluge akizungumza nafasi ya sheria katika suala hilo, alisema hakuna sheria inayozungumzia kwamba kutupa viungo vya binadamu au mwili hadharani ni kosa.
Mluge alisema jamii lazima itofautishe Sheria na suala zima la maadili na ubinadamu. Alisema kibinadamu na maadili, utupaji wa viungo vya binadamu si sahihi na ni jambo linaloshitua lakini kisheria, haimtii mtu hatiani . “Kimaadili si sawa, lakini suala hili ni la kiubinadamu halina sheria,” alisisitiza.
Alisema hata mtu anapokutwa na kiungo cha binadamu, hatiwi hatiani kwa maana ya kukutwa na kiungo husika isipokuwa, kinachotafutwa ni kujiridhisha ni kwamba amekipataje kutoka mwili wa binadamu.“Si kosa kukutwa na kiungo cha binadamu…cha msingi, ni kuthibitisha umekipataje,” alisema.
Vyuo hupataje miili
Kumekuwepo maswali juu ya ni namna gani vyuo vinapata miili ya kufanyia mafunzo kwa vitendo na baada ya mafunzo inapaswa iteketezwe namna gani.
Hata hivyo katika kutafuta ufafanuzi wa maswali haya, taasisi hizo zinazohusika na usimamizi wa vyuo hazikuwa tayari kuzungumzia kwa undani suala hilo, kwa madai ya kusubiri matokeo ya tume iliyoundwa.
Tume hiyo iliyoundwa, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, itahakikisha inakuja na majibu, ikiwa ni pamoja na kujua idadi kamili ya watu wenye viungo hivyo.
Timu hiyo ya wataalamu ya watu saba inayohusisha pia Mkemia Mkuu wa serikali, itakuja na majibu viungo hivyo ni vya muda gani na zilitumika kemikali gani kuvikausha. Jopo litabaini pia kama ipo sheria na ni ipi inavunjwa.
Inalenga kubaini pia kama upo uzembe katika kulinda viungo vya binadamu na vinapatikanaje kwa ajili ya mazoezi.
Katika sakata hilo lililovuta hisia za watu na kuzua mjadala mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo Madaktari wa IMTU, walikamatwa juzi na Polisi kwa mahojiano wakituhumiwa kuhusika katika utupaji viungo vya binadamu jalalani.
Polisi ilisema mifuko ipatayo 85 yenye vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu, ilikutwa maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji, eneo la Bunju jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment