skip to main |
skip to sidebar
MFUNGWA SAJINI RHODA ROBERT ALIYEMUUA MTOTO WA FUNDIKIRA AMEFARIKI DUNIA AKISUBIRI KUNYONGWA
Mfungwa aliyemuua mtoto wa Fundikira afariki dunia
- Ni askari wa JKT aliyekuwa akisubiri adhabu ya kunyongwa
- Azikwa na Magereza kwa mujibu wa sheria badala ya ndugu
Mfungwa Sajini Rhoda Robert aliyekuwa anasubiri adhabu ya kunyongwa kwa kosa la kumuua mtoto wa kigogo Swetu Fundikira, amefariki dunia wakati akitibiwa katika hospitali ya mkoa ya Dodoma, kufuatia hali yake kubadilika kutokana na kuishiwa damu mwilini.
Rhoda aliyekuwa askari wa kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mbweni na wenzake Koplo Ally Ngumbe na Mohamed Rashid, walihukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mtoto wa Chifu Abdallah Fundikira.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Zainabu Muruke Novemba 20, 2012.
Hadi mauti yanamkuta, Jaji Muruke aliyesikiliza na kutoa hukumu ya kesi hiyo alikuwa hajasaini hukumu hiyo na kuwafanya wafungwa hao kushindwa kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo.
Mapema mwaka huu wakili wa wafungwa hao, Kaloli Muruge, aliiambia NIPASHE kuwa aliwasilisha kusudio la kukata rufaa lakini kikwazo ilikuwa ni nakala ya hukumu ambayo jaji alikuwa hajaisaini.
Habari za kuaminika kutoka Gereza la Isanga mkoani Dodoma ambapo mfungwa huyo alikuwa akisubiri kunyongwa, zilisema kuwa Sajenti Rhoda alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akisumbuliwa na maradhi.
Alisema hali ya mfungwa huyo ilibadilika na kufariki dunia akiwa hospitalini hapo.
“Alizikwa gerezani kwa sababu alikuwa ni mfungwa ambaye kisheria hairuhusiwi kuzikwa uraiani lakini mwishoni mwa wiki ndugu zake waliarifiwa kuhusu kifo chake kabla ya mazishi na walifika na kuonyeshwa kaburi lilipo,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
NIPASHE ilizungumza na Mkuu wa Gereza la Isanga, Makoti Mwaibale, ambaye alithibitisha kufariki kwa mfungwa huyo. Alisema mfungwa huyo alifariki dunia Juni 20, mwaka huu katika hospitali hiyo akiwa anapatiwa matibabu.
Alisema Rhoda aliumwa na kupelekwa hospitalini Juni 15, mwaka huu ambapo alilazwa huku akiendelea na matibabu kwani ugonjwa uliokuwa unamkabili ulimsababishia kupungua kwa damu.
"Ugonjwa wa mtu ni siri hivyo alikuwa akiongezewa damu na ilipofika Juni 20 majira ya saa 1 asubuhi alifariki dunia," alisema. Mwaibale alisema mfungwa huyo alizikwa siku hiyo katika makaburi ya wafungwa yaliyopo Dodoma.
Alisema mume wa marehemu pamoja na mjomba wake walitaka kuuchukua mwili huo kwa ajili ya mazishi lakini haikuwezekana kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, alisema kwa mfungwa ambaye amehukumiwa kunyongwa hadi kufa akifariki anazikwa na magereza lakini angekuwa ni mahabusu wa kawaida mwili huo ungekabidhiwa kwa ndugu zake.
Alisema ndugu wa marehemu hawakushirikishwa katika mazishi kwa kuwa kuna sheria zinazowaongoza katika jambo hilo.Mwaibale alisema ndugu zake akiwamo mume wake walifika Juni 22, na kuonyeshwa kaburi la mfungwa huyo lilipo.
Hukumu ya askari hao ilisomwa na Jaji Muruke alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndiyo waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka hayo.
Alisema kuwa anakubaliana na mtiririko wa ushahidi wa upande wa mashtaka kama ulivyoelezwa na mashahidi wake sita akiwemo daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu pamoja na askari polisi wawili ambao washtakiwa katika utetezi wao walishindwa kuuvunja.
“Sheria iko wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa mara ya mwisho na baadaye mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndiyo unawajibika kutoa maelezo ya kina kuhusu yaliyompata mtu huyo,” alisema Jaji Muruke na kuongeza;
“Kisheria ukitoa maelezo ambayo hayajakidhi haja na yana utata ni faida kwa upande wa mashtaka ambao hutegemea ushahidi wa mazingira. Maelezo ya kina hayajatolewa na washtakiwa wote.”
Aliendelea, “Ushahidi wa Jamhuri japokuwa ni wa mazingira, umejengwa thabiti na upande wa utetezi haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja mnyororo huo, kidole kinawaelekea wao.”
Jaji Muruke alisisitiza kuwa katika kesi hiyo licha ya kuwa kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka.
Sajini Roda na Koplo Mohamed Rashid wote wa JKT Mbweni na Koplo Ally Ngumbe (37) wa Kikosi cha JWTZ Kunduchi, walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka huu saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki dunia usiku huohuo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment