Pages

Monday, 28 July 2014

MAMA KIKWETE AWATAKA WANAWAKE WENYE UGONJWA WA FISTULA KUJITOKEZA NA KWENDA KUPATA MATIBABU

Mama-Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo aliyekuwa Lindi
28/7/2014 Wanawake wenye tatizo la ugonjwa wa Fistula wametakiwa kutokuogopa na kukaa kimya bali wajitokeze  hadharani kwa kwenda Hospitali kupata matibabu  au kuwaambia viongozi wao ili waweze kuwasaidia kwani ugonjwa huo unatibika na matibabu yake ni bure.


Rai hiyo imetolewa  hivi karibuni na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya chama hicho  katika matawi ya Mkoimba, Ng’apang’apa, Mbuyuni B, Mkanga, Mtutu na Rutende.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema ugonjwa wa Fistula unatokana na uzazi, mwanamke akishikwa na uchungu wa kujifungua kwa muda mrefu kibofu cha mkojo kinaharibika na mgonjwa  hutokwa na haja ndogo mara kwa mara bila kutegemea.
“Mnapoona katika jamii yenu kuna mwanamke anatatizo hili muwasiliane na uongozi wa wilaya ili tuweze kumsaidia mama huyu kwa  kumpeleka Hospitali ya CCBRT ambako atafanyiwa upasuaji na kurudi katika hali yake ya kawaida kama alivyokuwa zamani”, alisema Mama Kikwete.
Kuhusu ugonjwa wa saratani aliwasisitiza viongozi hao kuwa wajumbe wazuri ili wawahimize wanawake kujitokeza kwa wingi kupima saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwani  kina mama wengi wanakufa kutokana na ugonjwa huo kwani unatibika endapo mgonjwa  atawahi kupata  matibabu .
Alisema , “Nanyi Kina baba muwasisitize na kuwapa ushirikiano wake zenu ili waende kupima na kama utaona mkeo anadalili za saratani ya kizazi awahi Hospitali mapema kupata matibabu.
“Kina mama mkienda Hospitali waombeni  wauguzi wawaelekeze jinsi ya kupima saratani ya matiti, ni rahisi na   hii itakusaidia hata wewe mwenyewe kujipima unapokuwa nyumbani”.
Kwa upande wa kina mama wajawazito aliwasihi  kuhudhuria kliniki  mapema ili kama kuna tatizo litagundulika mapema na kupelekwa katika Hospitali kubwa na hivyo kujifungua salama pia watapewa dawa za kumeza ambazo mama mjamzito anatakiwa kuzitumia.
Aidha MNEC huyo aliwasisitiza wanawake kujitokeza  kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani ili waweze kufika ngazi ya maamuzi na kuweza kuwatetea wanawake na watoto ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.
Akizungumzia kuhusu malezi ya watoto Mama Kikwete aliwataka wazazi na walezi kuwalea watoto wao  katika misingi mizuri ya dini na kuwapeleka shule wakapate elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao pia msiwafiche watoto wenye tatizo la ugonjwa wa mdomo sungura ambao unatibika kwa njia ya upasuaji.
Wakati huohuo Mama Kikwete akiwa katika matawi hayo alipata muda wa  kuwapa nasaha  watoto waliofika kumsalimia kwa kuwahimiza umuhimu wa kusoma kwa bidii kwani elimu ndiyo kitu pekee kitakachowasaidia kujikwamua kiuchumi katika maisha yao ya  baadaye.
“Wazazi wenu wanapowaamsha asubuhi ili muende shule kwa sasa baadhi yenu mnaona kama wanawasumbua vumilieni hii tabu mnayoipata sasa , mtakuja kufaidi matunda yake hapo baadaye pale mtakuwa mmemaliza masomo yenu na kupata kazi”, alisisitiza Mama Kikwete.
MNEC huyo ambaye alikuwa wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao vya ndani na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 akiwa katika tawi la Mbuyuni B aliwakabidhi kadi wanachama wapya wa CCM tisa na Umoja wa Wanawake (UWT) watatu

No comments:

Post a Comment